Usawiri wa Familia ya Kisasa katika Fasihi ya Watoto Nchini Kenya

Authors

  • Gatere Lucy Njeri Chuo Kikuu cha Nairobi Author
  • James Omboga Zaja Chuo Kikuu cha Nairobi Author
  • Rayya Timammy Chuo Kikuu cha Nairobi Author

Keywords:

Fasihi ya Watoto, Familia, Usawiri, Familia Kiini, Watoto

Abstract

Madhumuni ya makala haya ni kuhoji kwamba licha ya kuwepo kwa familia za aina mbalimbali na zilizo changamano nchini Kenya, watunzi wa hadithi za watoto wanaendelea kusawiri familia kiini ambazo kimsingi huwa na baba, mama na watoto, ilhali kihalisia wapo watoto wanaotokana na familia za mzazi mmoja, familia za malezi na wengine kutoka taasisi za malezi na hata familia ambapo walezi wa watoto ni babu na nyanya za watoto wanaolelewa. Kwa misingi hii kunaweza kutolewa hoja kwamba fasihi ya watoto ya kisasa nchini Kenya haiwasilishi upana, uchangamano na usasa wa kifamilia kwa sababu tathmini za hadithi nyingi za watoto zilizoko zinadhihirisha uhalisi wa usawiri wa familia wa aina moja na kwa hivyo kuibua fikra potovu kwamba watoto kama wahusika katika tungo mbalimbali za fasihi ya watoto wanatoka katika familia zinazowiana. Uhalisi huu wa chukulizi potovu za uwepo wa familia kiini katika hadithi za watoto unadhihirika katika vitabu viwili teule vya fasihi ya watoto - ‘Mwepesi wa Kusahau’ na ‘Likizo ya Mkosi.’ Usawiri wa familia katika vitabu hivi umekitwa katika uelewa banifu kwamba kimsingi, familia huendesha shughuli za kila siku kama familia kiini - yaani familia inayojumuisha baba, mama na watoto, familia isiyokuwa na mahusiano na familia pana. Makala haya yanapania kupendekeza kwamba utunzi wa hadithi za watoto unahitaji ujasiri wa kusawiri mifumo anuwai ya kifamilia inayojitokeza katika hadithi za watoto katika upana wake wa kiuchangamano ili kuwezesha kuakisika kwa mifumo na miundo yote ya kifamilia inayopatikana nchini Kenya. Hii itawezesha usomaji wa fasihi ya watoto shuleni kwenda hatua zaidi ya burudani na kutilia mkazo usomaji unaojenga ukuaji wa mitazamo chanya ya maisha miongoni mwa watoto wakiwa wangali wadogo kuhusiana na usawiri wa familia. Makuzi ya watoto na ufunzaji wa maadili ni mambo yawezekanayo sio katika misingi ya familia tu bali pia kupitia mafunzo ya fasihi ya watoto.

Downloads

Published

01-09-2020

Issue

Section

Articles