Sifa za Vitanzandimi vya Kiswahili katika Mawasiliano ya Jamii

Authors

  • Rashidi Abdallah Mwanyumbwe Shule ya Msingi Duthumi Author
  • Mussa Omari Amanzi Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro Author

Keywords:

Vitanzandimi, Fasihi Simulizi, Mawasiliano, Jamii, Kiswahili

Abstract

Vitanzandimi ni nui muhimu ya fasihi simulizi. Nui hii ina mnasaba wa moja kwa moja na jamii kulingana na zama, itikadi pamoja na utamaduni wa jamii ikiwemo mila, dasturi, mtindo wa maisha, ufundi wa aina zote na kadhalika. Utanzu huu wa semi katika fasihi simulizi una kazi lukuki katika jamii, miongoni mwa kazi hizo ni kutoa motisha kwa wanafunzi kutamka maneno (Morris, 1975). Kadhalika, vitanzandimi huleta raha kwa watu kwa sababu ndani yake mna marudio ya sauti fulani ambazo huleta ladha ya kimuziki na hata pale msemaji anaposhindwa kuyatamka maneno hayo (Wanjala, 2011). Hata hivyo, vitanzandimi kama utanzu muhimu wa semi huiburudisha jamii hasa watoto (Wamitila, 2004). Licha ya umuhimu na kazi kubwa ifanywayo na vitanzandimi katika jamii, nui hii ya fasihi simulizi bado haijafafanuliwa kwa kiwango cha kutosha katika lugha ya Kiswahili. Hii ni kwa sababu ya kutoelezwa kwa uwazi sifa za maneno hayo (vitanzandimi) zaidi ya kudokezwa kijumla tu kupitia fasili zilizotolewa na wataalamu mbalimbali wa fasihi. Kadhalika, kumekuwa na utofauti na mwachano mkubwa wa mifano ya vitanzandimi kutokana na miegamo ya fasili za vitanzandimi zilizodokezwa na wataalamu mbalimbali wa fasihi. Kwani, baadhi ya wataalamu huamini kuwa vitanzandimi ni mchezo wa maneno, wengine huamini ni maneno yanayotatiza kimatamshi, na wengine wakiamini ni maneno yanayokaribiana sana kimaana na kisauti pale yanapotamkwa. Ingawa si jukumu wala lengo la makala yetu kushughulikia utofauti ama mwachano huo wa mifano ya vitanzandimi kutokana na miegamo hiyo ya fasili za vitanzandimi zilizodokezwa na wataalamu wa fasihi ‘la hasha’. Makala hii ilitia nanga katika kubainisha sifa zinazovitambulisha vitanzandimi vya Kiswahili katika mawasiliano ya jamii (watu). Hivyo, kupitia makala haya imebainika kuwa vitanzandimi vya Kiswahili vina sifa zake kadha wa kadha kutokana na uamilifu wake kwa jamii.

Downloads

Published

30-09-2023

Issue

Section

Articles