Usawiri wa Wahusika wa Jinsia ya Kiume katika Riwaya ya 'Chozi la Heri'
Keywords:
Fasihi, Uhalisia, Uhakiki, Jinsia, WahusikaAbstract
Fasihi ni kioo cha jamii kitumiacho lugha kwa usanii kwa kuashiria hali ya maisha katika jamii na kubainisha jinsi jamii inavyoshughulikia masuala mbalimbali. Makala haya inashughulikia usawiri wa wahusika wa jinsia ya kiume katika riwaya ya Chozi la Heri na Assumpta Matei. Lengo kuu la makala haya ni kuchunguza usawiri wa wahusika wa kiume katika riwaya na aidha, kubainisha mielekeo ya wanajamii kuwahusu wahusika wa kiume. Makala haya yalijikita katika madhumuni ya kueleza matatizo yanayowakumba wanajinsia ya kiume katika riwaya ya Chozi la Heri. Nadharia ya Uhalisia imeongoza mjadala huu. Nadharia hii, iliasisiwa na tapo la wanamaendeleo. Baadhi ya waasisi wa nadharia ya Uhalisia ni kama vile; Balzac, Stendhal na Flaubert. Nadharia ya Uhalisia hutumiwa na watunzi kumulika tajriba anuwai katika jamii. Matokeo ya makala haya yalionyesha kuwa wahusika wa jinsia ya kiume wanapitia matatizo kama vile; kubaguliwa, upweke, kuharibiwa kwa mali zao, kupokonywa ardhi, kuhujumiwa, kuingizwa katika ulanguzi wa dawa za kulevya, kuibiwa, kusalitiwa, kuchochewa na kutoajiriwa. Inatarajiwa kuwa matokeo ya makala haya yatawafaa wasomi, wanajamii, na waandishi kung’amua kuwa nyakati za kumtwaza mwanaume zimeisha kwani anakumbwa na matatizo sawa na apitiayo mwanamke.