Ukiushi wa Taswira Dumifu za Uana katika Ugavi wa Kazi na Majukumu
Tathmini ya Hadithi Teule za Kiswahili za Watoto
Keywords:
Taswira Dumifu, Uana (TDU), Kazi, MajukumuAbstract
Makala hii inachunguza ukiushi wa taswira dumifu za uana katika ugavi wa kazi na majukumu kwenye hadithi za Kiswahili za watoto. Lengo kuu hasa ni kupambanua namna ambavyo ugavi wa kazi na majukumu kwenye hadithi teule za Kiswahili za watoto umekiuka taswira dumifu za uana. Nadharia ya Udenguzi ilitumika kuwa kiunzi cha nadharia na vilevile katika uchanganuzi wa data. Utafiti huu ulizingatia muundo wa kimaelezo na mbinu ya uhakiki makinifu wa matini. Data iliyotumika katika makala hii ilitokana na uhakiki wa hadithi 11 za Kiswahili za watoto. Hadithi zilizochanganuliwa zilisampulishwa kimakusudi kwa kuzingatia malengo ya utafiti. Uwasilishaji wa matokeo ya utafiti ulifanywa kwa kutumia maelezo. Matokeo ya utafiti huu yanadhihirisha kuwa kazi kama vile ualimu, udaktari, uaskari, uanajeshi, urubani, ukulima, uhadhiri, ufanyi biashara, na uhakimu ulifanywa na wahusika wa kike. Aidha, majukumu kama vile kulima, kufyeka, kusukuma toroli, kulisha ng’ombe, na kuchunga mifugo yalifanywa na wahusika wa kike huku wahusika wa kiume wakitekeleza majukumu kama vile kuosha vyombo na kuandika meza. Kwa kuhitimisha, matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa taswira dumifu za uana zimekiukwa katika ugavi wa kazi na majukumu, kwenye hadithi za Kiswahili za watoto. Makala hii hivyo basi inapendekeza matibaa, mashirika ya kuchapisha vitabu vya watoto na asasi za kiserikali zibuni sera na miongozo itakayohakikisha kuwa taswira dumifu za uana zinadhibitiwa hususan katika ugavi wa kazi na majukumu. Mwisho, makala hii pia imedhihirisha kuwa fasihi ya Kiswahili ya watoto ni nyenzo muhimu katika Jitihada za utatuzi wa migogoro ya kiuana ambayo huathiri mahusiano ya kijinsia katika jamii.