Usawiri wa Wahusika wa Kike katika Tamthilia za 'Sudana' na 'Dunia Hadaa'

Authors

  • John Mutua Chuo Kikuu cha Machakos Author
  • Rocha Chimerah Chuo Kikuu cha Pwani Author
  • Nancy Ngowa Chuo Kikuu cha Pwani Author

Keywords:

Chanya, Mtazamo, Mwanamke, Ufeministi wa Baada Ukoloni, Mhusika

Abstract

Suala la mahusiano ya wanawake na wanaume ulimwenguni limekuwa na linaendelea kuwafikirisha wahakiki na wanafasihi kote duniani kwa karne nyingi. Katika kuikabili kadhia hii, kumeibuliwa nadharia na mitazamo mbalimbali inayojaribu kueleza namna ya kuleta maridhiano ili kutuliza mgogoro baridi usiosita kwa kusudi la kutafuta usawa wa kijinsia. Mtazamo unaohusishwa na mhakiki wa kimarekani, Mary Ellman katika kitabu chake Thinking about Women, mwandishi huyo alielekea kughadhabishwa na jinsi mwanamke alivyosawiriwa katika kazi zilizoandikwa na waandishi wanaume. Aidha, aliangazia jinsi baadhi ya waandishi wa kike wanavyoendeleza usawiri huo hasi wa wanawake katika kazi zao. Mawazo ya Ellman yaliungwa mkono na Millet (1970) katika Sexual politicsalipowashambulia waandishi wa kiume kwa kuwasawiri wahusika wao wa kike kwa mtazamo hasi. Hali hii inachochea fikira kwamba waandishi wa kiume huwasawiri wahusika wa kike kwa namna tofauti wakilinganishwa na waandishi wa kike. Ikiwa kauli hiyo ina mashiko, basi itakuwa sawa kudai kuwa waandishi wa kiume ndio wa kulaumiwa kwa kuendeleza usawiri mbaya (hasi) kwa wahusika wa kike. Pia, ni sawa kudai kuwa waandishi wanawake wanawasawiri wahusika wa kike kwa mtazamo mzuri (chanya). Lengo la makala haya ni kulinganisha usawiri wa wahusika wa kike katika tamthilia ya Sudana ya Mazrui na Njogu (2006) na Dunia Hadaa ya Kisovi, (2007) ambazo zimeandikwa na waandishi wa jinsia tofauti. Makala haya yanakisia kuwa pana uhusiano wa karibu baina ya jinsia ya mwandishi na usawiri wa mhusika wa kike. Pia, tunachukulia kuwa pindi mitazamo ya waandishi hawa itakapobainishwa itasaidia kukadiria uwezekano wa fasihi kuwa chombo madhubuti katika kufikia usawa wa kijnsia. Ili kufikia lengo hili, tumeongozwa na nadharia ya Ufeministi wa Baada-ukoloni. Nadharia hii imetuwezesha kutambua sifa za mwanamke mwafrika akisawiriwa na waandishi waafrika.

Downloads

Published

30-09-2021

Issue

Section

Articles