Nafasi ya Sheng katika Utangazaji wa Biashara Jijini Nairobi
Keywords:
Biashara, Sheng, Mazungumzo, UtangazajiAbstract
Makala haya yanabainisha nafasi ya Sheng katika utangazaji wa biashara jijini Nairobi. Kichocheo cha utafiti huu kilikuwa kuwepo na chukulizi mpya kwamba Sheng imejitanzua kutoka kwenye upembezwaji na kuingia katika matumizi mapya yaliyo kinyume na chukulizi za awali kuwa ni lugha chafu na ya wahuni. Malengo yalikuwa kubainisha sababu ambazo zimefanya Sheng kutumika katika utangazaji wa biashara jijini Nairobi na kiwango cha matumizi yake katika utangazaji wa kibiashara jijini Nairobi. Nadharia mbili zimetumiwa kuchanganua data tuliyoipata nyanjani. Nadharia hizi ni ile ya Mchezo iliyoasisiwa na Neumann na Oskar Morgenstern (1944) na kuendelezwa na wasomi wengine kama vile Peter (2015) na Samuelson (2016), na Nadharia ya Maafikiano ya Mazungumzo iliyoasisiwa na Mwingereza Giles na wengine (1970). Tumetumia mbinu za mahojiano, kujaza hojajji, upigaji picha na uchunguzi shiriki ili kupata data tuliyolenga. Matokeo ya utafiti huu yameonyesha kuwa Sheng hutumiwa zaidi na vijana kutangazia biashara jijini Nairobi kutokana na sababu mbalimbali. Isitoshe, imebainika kuwa nafasi ya Sheng katika utangazaji wa biashara jijini Nairobi hutegemea hadhira au wateja wanaolengwa hasa vijana, bidhaa zinazouzwa na sehemu ambako biashara inaendeshewa.