Utata katika Uainishaji wa Fasihi Simulizi
Hali ya Sasa na Mustakabali Wake
Keywords:
Tanzu, Vipera, Mafumbo, Maigizo, Mazungumzo na MivighaAbstract
Makala haya yanajadili suala la vigezo vinavyotumiwa kuainisha fasihi simulizi katika lugha tofautitofauti. Utafiti wetu ulichochewa na masuala kadha: Je, baadhi ya maumbo yaliyozoeleka kuitwa tanzu au vipera vya Fasihi Simulizi ni sehemu ya Fasihi? Yaani, mafumbo, michezo jukwaani, mawaidha, maigizo, mazungumzo na mivigha ni tanzu au vipera vya Fasihi Simulizi kweli? Je, katika lugha nyinginezo, ‘tanzu’ au ‘vipera’ hivi vipo na vinaitwaje? Je, fasihi ni nini? Katika kujibu maswali haya na mengine, makala haya yanabainisha kwamba, masuala haya sita sio vipera wala tanzu za Fasihi Simulizi bali, mengine ni majukumu ya Fasihi Simulizi; mbinu zinazotumiwa kuwasilisha Fasihi Simulizi; na majukwaa yanayoruhusu utendaji wa Fasihi Simulizi. Kwa kuongozwa na Nadharia ya Tanzu, mfano mzuri ni ‘utanzu’ unaoitwa ‘mivigha’ haupo; badala yake ‘utanzu’ huu unafaa kuangaliwa kama jukwaa linaloruhusu utolewaji wa tanzu mbalimbali zinazoingiliana katika utendaji. Hii ni kwa sababu, mivigha ni sawa na basi linalobeba tanzu na vipera kama abiria kuelekea sehemu mbalimbali. Hii ina maana kuwa, ‘mivigha’ sio utanzu wala kipera bali ni kongoo la Fasihi Simulizi linaloelea na ambalo ‘tanzu’ mbalimbali hupanda jukwaani na kutekeleza wajibu wake, na baadaye kushuka au kushushwa ili kupisha tanzu zingine; nazo zitekeleze wajibu wake. Upandaji na ushukaji huu wa tanzu hizi huiwezesha mivigha husika kutekeleza wajibu wake wa ujumla.