Sanaajadiiya Mtandaoni
Misimbo Ibuka Yaimarika ilhali Kiswahili Chaganda
Keywords:
Sanaajadiiya, Sheng, Mchongoano, Methali, Fasihi SimuliziAbstract
Kama lugha nyinginezo, ubunifu ulioandamana na ngoma za jadi, mashairi, miiko, ngano na masimulizi mengineyo katika lugha ya Kiswahili ulididimia na sanaa hii ikagandama pale tanzu mbalimbali zilipoandikwa kwenye vitabu. Kiswahili kiliposambaa kutoka Uswahilini, hakikujumuisha kimamilifu sanaajadiiya ya tamaduni za wakaazi wa bara. Hivyo basi kumekuwa na haja ya uwiano kati ya sanaajadiiya ya Kiswahili na ile ya tamaduni nyinginezo. Makala haya yanauangaza msimbo ibuka wa Sheng na jinsi umekuwa kielelezo kizuri cha namna vipengele vya lugha ya Kiswahili vinaweza kufinyangwa upya na kuendelezwa ili kusawiri uhalisia wa watumizi wa lugha. Makala inadai kuwa Kiswahili kimeganda katika uwanja wa sanaajadiiya na nafasi yake kuchukuliwa na Sheng hasa katika matumizi ya TEHAMA. Tanzu nne za sanaajadiiya ya Sheng zitajadiliwa; mchongoano, ujinga ni…, methali, na uvumi. Makala haya yatajaribu kujibu maswali kama vile; Je, tanzu hizi ni upotovu wa nidhamu au ni sanaa yenye nafasi yake katika utagusano wa kijamii? na je, ni kwa kiasi gani tanzu hizi za sanaajadiiya zimefanikiwa kutekeleza majukumu yanayotekelezwa na sanaa kwa jumla? Makala yanapendekeza ukubalifu wa misimbo ibuka itakayowasilisha uhalisia wa mikatadha tofauti ya Kiafrika ili kukifanya Kiswahili kukubalika katika sehemu tofauti za Afrika.