Uamili wa Ngazi ya Utambuzi katika Riwaya za Kiswahili

Authors

  • Dinah Sungu Osango Chuo Kikuu cha Nairobi Author
  • Mwenda Mbatiah Chuo Kikuu cha Nairobi Author
  • Rayya Timammy Chuo Kikuu cha Nairobi Author

Keywords:

Ufokasi, Nadharia ya Naratorojia, Ngazi ya Utambuzi, Uamili

Abstract

Makala haya yanaangazia na kuchunguza dhana ya ngazi ya utambuzi na uamili wake katika riwaya za Kiswahili zilizoteuliwa makusudi kuukita na kuuendeleza mjadala unaodhamiriwa katika makala haya. Ngazi ya utambuzi ni mojawapo ya ngazi mbalimbali za ufokasi zilizopendekezwa na wananaratolojia kama vile Uspensky (1973) na Rimmon-Kenan (1983). Kimsingi, ufokasi ni mtazamo ambao huchukuliwa katika kuwasilisha simulizi na kuikuza hadithi tawala kwa ujumla. Ufokasi unajishughulisha kubaini ni nani anayeona kinachosimuliwa katika simulizi. Ufokasi ni istilahi iliyobuniwa na wananadharia ya naratolojia kurejelea kile ambacho katika uhakiki wa kijadi kilijulikana kama kitazamio. Abrams (1993) anaifafanua dhana hii ya ufokasi kuwa inarejelea jinsi hadithi inavyowasilishwa yaani, njia ambazo mwandishi anazitumia kusawiri na kuwasilisha kwa msomaji wahusika, dayalojia, matendo, mandhari na matukio yanayounda simulizi katika kazi ya bunilizi. Kwa upande wake, Hawthorn (2010:122) anasema kwamba, istilahi ya “kitazamio” haipambanui ni nani msemaji na nani anayeona na nini anachoona katika simulizi. Hii ndiyo sababu Genette (1972) alibuni istilahi hii ya ufokasi kama mkakati wa kuwezesha kutambua na kutofautisha kati ya msemaji na mfokasi katika simulizi za kifasihi. Kwa kujikita katika dhana hii ya ufokasi, msomaji au mchanganuzi anaweza kutambua pale ambapo mwandishi ndiye aliyeyashuhudia au anayeyashuhudia matukio au pale ambapo mwandishi anamtumia mmojawapo wa wahusika kuwasilisha ujumbe wake. Ili kutuwezesha kubainisha uamili wa ngazi ya utambuzi katika riwaya ya Kiswahili, data ya kuudhibiti na kuthibitisha madai ya mjadala tawala itatolewa katika riwaya za Kiswahili zilizoteuliwa makusudi zikijumuisha (C.S.L. Chachage, 2005), Nyuso za Mwanamke (S.A. Mohamed, 2010), Harufu ya Mapera (K. W. Wamitila, 2012), Hujafa Hujaumbika (F.M. Kagwa, 2018), Haini (Adam Shafi, 2002), na Ndoto ya Almasi (Ken Walibora, 2006). Uteuzi wa riwaya hizi unahalalishwa kwa misingi kwamba, hizi ni riwaya zilizo na matini pana zinazowezesha udondoaji wa mifano faafu inayodhihirisha ngazi za ufokasi na wakati huo huo kudhihirisha uamili wa ngazi hizo katika simulizi. Mjadala wa kimsingi katika makala haya umekitwa na kuongozwa na madai ya teneti za kimsingi za Nadharia ya Naratolojia ambayo inatambua ufokasi na uhusika kama vipengele muhimu katika uwasilishaji wa simulizi.

Downloads

Published

30-04-2024

Issue

Section

Articles