Changamoto za Kuingiza Antonimu katika Kamusi Wahidiya za Kiswahili
Mifano kutoka Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la Tatu (KKK3)
Keywords:
Antonimu, Nadharia Jumuishi ya Leksikografia, Vidahizo, Kamusi WahidiyaAbstract
Makala haya yamechunguza changamoto za kuingiza antonimu katika fasili za vidahizo vya kamusi wahidiya za Kiswahili. Data zilikusanywa maktabani kwa njia ya usomaji matini. Matini iliyosomwa kwa ajili ya mifano ni Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la Tatu (KKK3). Vidahizo 379 kati ya 22675 vya KKK3 vilibainika kuwa vimetumia antonimu kufafanua maana zake. Vidahizo vilivyokusanywa vilitumika kama data kushadidia hoja. Data hizo zimechanganuliwa kwa kutumia mikabala ya kitaamuli na kitakwimu. Aidha, Nadharia Jumuishi ya Leksikografia aliyoiasisi Herbert Wiegand imeongoza uchanganuzi wa data. Nadharia hii imeegemea kwenye misingi inayohusu kujali mahitaji ya walengwa wa kamusi, matumizi ya maarifa ya nadharia nyingine nje ya leksikografia na kuangalia kamusi kwa kuzingatia kanuni asilia za wanaleksikografia tangulizi. Makala yamebainisha changamoto za antonimu kileksikografia. Mosi, ni kubadilika kwa kategoria ya kidahizo na antonimu. Pili, ni ukosefu wa urari wa idadi ya antonimu ndani ya kitomeo. Tatu, ni ukosefu wa urari wa mpangilio wa antonimu ndani ya vitomeo. Nne, ni kutozingatia alama za uakifishi. Tano, ni kuwapo kwa upendeleo wa kileksikografia. Sita, ni mpishano wa kidhana kati ya kidahizo na ufafanuzi wake unaohusu antonimu. Makala yanapendekeza watungaji wa kamusi wazingatie kanuni za kufafanua vidahizo vya kiantonimu kwa namna isiyomsumbua mlengwa wa KKK3 kuzing’amua maana zilizokusudiwa kumfikia.