Athari za Mazingira Asilia ya Mtunzi katika Ukiushi wa Kaida za Uhalisia kama Kipengele cha Uhalisiamazingaombwe: Mifano kutoka Riwaya za Shaaban Robert na za Euphrase Kezilahabi
Keywords:
Ukiushi, Riwaya, Uhalisiamazingaombwe, MtunziAbstract
Makala haya yanachunguza jinsi ukiushi wa kaida za uhasilia kama kipengele cha uhalisiamazingaombwe unavyojitokeza katika riwaya za Shaaban Robert na za Euphrase Kezilahabi. Riwaya zilizoteuliwa ni Kusadikika (1951) na Adili na Nduguze (1952) za Shaaban Robert pamoja na Nagona (1990) na Mzingile (1991) za Euphrase Kezilahabi. Tumefanya uteuzi wa kazi mbili za Shaaban Robert na mbili za Kezilahabi ili kupata kazi zinazosadifu matumizi ya ukiushi wa kaida zilizoandikwa kabla na kipindi cha usasabaadaye katika fasihi ya Kiswahili. Kazi za Shaaban Robert zilizoteuliwa zimewakilisha kipindi kabla ya usasabaadaye na za Kezilahabi zimewakilisha kipindi cha usasabaadaye katika riwaya ya Kiswahili. Tumechagua riwaya zilizoandikwa katika vipindi hivyo tofauti ili kuchunguza jinsi ukiushi wa kaida kama kipengele cha uhalisiamazingaombwe ulivyotumika katika nyakati tofauti katika historia ya riwaya ya Kiswahili. Hii ni kwa sababu suala au tukio fulani linaweza kuonekana la ukiushi wa kaida au la kawaida kulingana na mabadiliko yanayotokea katika jamii uhusika. Mabadiliko hayo yanaweza kusababishwa na miingiliano ya jamii kiutamaduni pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Riwaya za Adili na Nduguze na Kusadikika za Shaaban Robert zimeteuliwa kwa sababu ndizo riwaya zake zilizosheheni matumizi mengi ya ukiushi wa kaida zenye sifa za uchawi na mazingaombwe zaidi ya riwaya zake zilizosalia; Ilihali riwaya za Nagona na Mzingile licha ya kusheheni matumizi mengi ya ukiushi wa kaida lakini ndizo riwaya za Kezilahabi zilizoandikwa kipindi cha usasabaadaye katika fasihi ya Kiswahili. Makala imejikita katika kuchunguza ukiushi wa kaida za mahali au mazingira, ukiushi wa kaida kati ya mbali na karibu, ukiushi wa kaida za kimawasiliano kwa kutumia lugha kati ya binadamu na viumbe wengine na ukiushi wa kaida kati ya uhai na kifo.