Mwingilianomatini katika Utanzu wa Riwaya
Mshabaha kati ya 'Nyuso za Mwanamke' na 'Wenye Meno'
Keywords:
Mwingilianomatini, Riwaya, Usemezano, UtunziAbstract
Kazi za kifasihi huhusiana, hurejeleana na huingiliana katika mchakato wa kuandikwa kwake, lakini mambo haya hujibainisha kwa uwazi zaidi katika mchakato wa upokezi na ufasiri wa kazi hizo. Bakhtini, mwasisi wa Nadharia ya Mwingilianomatini, anahoji kwamba utanzu wa riwaya una uwezo na wasifu wa kutumia na kushirikisha kiutunzi nduni za tanzu nyingine na bado utanzu huu ukabakia na sifa zake kama utanzu. Kwa mfano, riwaya inaweza kuhusisha na kushirikisha kiutunzi sifa au nduni ya mazungumzo ambayo aghalabu hubainika katika utanzu wa tamthilia au ikahusisha kanuni za ushairi na bado ikabakia kama riwaya. Mnadharia huyu anasema kwamba utanzu wa riwaya una upekee kwa sababu una uwezo wa kuchota sifa, mbinu na mikakati ya kiutunzi ya tanzu nyingine na kuzijumlisha katika kurutubisha muundo na usanifu wake kwa njia anuwai. Sifa hizi za kuhusiana, kurejeleana na kuingiliana kwa nduni za kiutunzi, ni uhalisia unaojitokeza kwa wingi katika tungo za Said Ahmed Mohamed. Kauli hii inahalisi kuhoji kuwa kuna kiasi kikubwa cha mwingilianomatini kinachojitokeza katika kazi za mtunzi huyu. Hali hii inashawishi na kuchochea shauku ya kiutafiti kutaka kubaini kama Said Ahmed anajikariri kiutunzi au kama kuakisika kwa nduni sawia kutoka kazi moja hadi nyingine ni ufundi wa kukuza na kuimarisha mbinu zake za kiutunzi. Hivyo, mchango wa makala hii katika kuziba pengo hilo ni kuchunguza jinsi riwaya mbili za Said Ahmed: Nyuso za Mwanamke (2010) na Wenye Meno (2014) zinavyoingiliana katika vipengele vya maudhui na uhusika. Usampulishaji wa kimakusudi umetumika kuteua kazi hizi. Kwa ujumla, mwelekeo wa makala ni wa mwingilianomatini.