Athari za Mazingira Asilia ya Mtunzi katika Ukiukaji wa Kaida za Uhalisia kama Kipengele cha Uhalisiamazingaombwe katika Riwaya za Shaaban Robert na za Euphrase Kezilahabi
Keywords:
Mazingira Asilia, Uhalisiamazingaombwe, UsasabaadayeAbstract
Makala haya yanachunguza jinsi ukiukaji wa kaida za uhasilia kama kipengele cha uhalisiamazingaombwe unavyojitokeza katika riwaya za Shaaban Robert na za Euphrase Kezilahabi. Riwaya zilizoteuliwa ni Kusadikika (1951) na Adili na Nduguze (1952) za Shaaban Robert pamoja na Nagona (1990) na Mzingile (1991) za Euphrase Kezilahabi. Tumefanya uteuzi wa kazi mbili za Shaaban Robert na mbili za Kezilahabi ili kupata kazi zinazosadifu matumizi ya ukiukaji wa kaida zilizoandikwa kabla na kipindi cha usasabaadaye katika fasihi ya Kiswahili. Kazi za Shaaban Robert zilizoteuliwa zimewakilisha kipindi kabla ya usasabaadaye na za Kezilahabi zimewakilisha kipindi cha usasabaadaye katika riwaya ya Kiswahili. Tumechagua riwaya zilizoandikwa katika vipindi hivyo tofauti ili kuchunguza jinsi ukiukaji wa kaida kama kipengele cha uhalisiamazingaombwe ulivyotumika katika nyakati tofauti katika historia ya riwaya ya Kiswahili. Hii ni kwa sababu suala au tukio fulani linaweza kuonekana la ukiukaji wa kaida au la kawaida kulingana na mabadiliko yanayotokea katika jamii uhusika. Mabadiliko hayo yanaweza kusababishwa na miingiliano ya jamii kiutamaduni pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Riwaya za Adili na Nduguze na Kusadikika za Shaaban Robert zimeteuliwa kwa sababu ndizo riwaya zake zilizosheheni matumizi mengi ya ukiukaji wa kaida zenye sifa za uchawi na mazingaombwe zaidi ya riwaya zake zilizosalia; Ilihali riwaya za Nagona na Mzingile licha ya kusheheni matumizi mengi ya ukiukaji wa kaida lakini ndizo riwaya za Kezilahabi zilizoandikwa kipindi cha usasabaadaye katika fasihi ya Kiswahili. Makala imejikita katika kuchunguza ukiukaji wa kaida za mahali au mazingira, ukiukaji wa kaida kati ya mbali na karibu, ukiukaji wa kaida za kimawasiliano kwa kutumia lugha kati ya binadamu na viumbe wengine na ukiukaji wa kaida kati ya uhai na kifo.