Istiara katika Riwaya ya 'Kusadikika' ya Shaaban Robert
Keywords:
Istiara, Riwaya, Kusadikika, Shaaban RobertAbstract
Makala haya yanakusudia kuonesha jinsi istiara ilivyotumika katika riwaya ya mwandishi nguli Shaaban Robert ambaye ni mmojawapo wa waandishi maarufu na waliosifika sana katika utunzi wa kazi mbalimbali za fasihi. Shaaban Robert aliiandika riwaya yake ya Kusadikika mnamo mwaka 1951. Utunzi wa kazi za fasihi kwa kutumia mbinu ya istiara ulikuwa/umekuwa nyenzo muhimu sana katika kuusawiri, kuubeza na kuukosoa mfumo wa kikoloni na pia hata mfumo mwingine wowote ule ambao unaonekana kwenda kinyume na matakwa ya jamii fulani. Kwa kuwa Shaaban Robert ni miongoni mwa watunzi wa kazi za fasihi walioanza kuandika kazi zao katika kipindi cha ukoloni, tumeona ni vyema tukaangalia ni kwa vipi mtunzi huyu ametumia mbinu hii ya istiara kama mbinu mojawapo za kiutunzi zenye lengo la kusawiri hali halisi katika jamii hususan katika kipindi cha ukoloni. Kwa hivyo basi, makala yatajikita katika kuangalia dhana ya istiara na jinsi ndugu Shaaban Robert alivyotumia istiara katika riwaya hii na pia kufafanua maana zinazoweza kupatikana kutokana na matumizi hayo ya istiara. Katika kufanikisha uchambuzi huu, makala haya yatatumia nadharia ya udenguzi kama ilivyoasisiwa na Derrida (1967).