Taswira kama Kurunzi ya Kuangazia Uozo katika Jamii ya Kisasa
Mfano kutoka Riwaya za 'Mafuta' na 'Walenisi'
Keywords:
Taswira, Kurunzi, Uozo, JamiiAbstract
Makala haya yanachunguza matumizi ya taswira kama kurunzi ya kuangazia uozo katika jamii ya kisasa kupitia riwaya za G.K Mkangi Mafuta (1984) na Walenisi (1995). Riwaya za Mafuta na Walenisi zinachunguza jinsi mfumo wa kisiasa unaodhibitiwa na tabaka la wachache unavyoweza kuathiri maisha ya wanaotawaliwa kijamii, kisiasa, kiuchumi, kidini na hata kisaikolojia. Zinaonyesha uozo uliopo katika tawala ambazo hazitilii maanani maslahi ya wengi. Makala haya yanachanganua taswira zilizotumiwa na Mkangi ili kubainisha uozo huu kupitia masuala ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kidini. Katika riwaya hizi, mwandishi Mkangi alitumia taswira kimakusudi ili kuepuka kupigwa marufuku kwa kazi zake. Katika mbinu hii kunatokota masuala nyeti ya kijamii na kisiasa ambayo alikusuadia kuyapitisha kwa msomaji wake. Matumizi ya taswira yalimwezesha kushambulia wenye mamlaka bila ya kuamsha hasira yao. Katika kufanya hivi, alitoa hadharani upungufu na uozo wa jamii yake na jamii pana ya ulimwengu. Alikuwa na lengo la kuamsha umma mpana unaolala kuhusu hali halisi ya maisha yao. Wakati ambapo alikuwa akiandika riwaya hizi, uhuru wa kujieleza na kuikosoa serikali iliyokuwa mamlakani ulidhibitiwa. Kazi zilizoonekana kuikosoa serikali zilipigwa marufuku. Hivyo basi, ni wazi kwamba Mkangi alibuni mbinu ya taswira ili iweze kuchukuana na mazingira na wakati. Mwandishi Mkangi aliyafumbika maswala nyeti katika mbinu ya taswira ili awasilishe vizuri zaidi ujumbe wake kwa jamii kwa njia halisi. Taswira alizozitumia zina nguvu kubwa ya kuganda akilini ili msomaji aweze kufafanukiwa na uhalisi wa hali yake na wakati huo huo kupata msukumo wa kubadilisha mfumo huo dhalimu.