Ujenzi wa Ujitambuzinafsi Hasi katika Bunilizi za Omar Babu
Keywords:
Bunilizi, Ujenzi, Upembezwaji, UjitambuzinafsiAbstract
Ujenzi wa ujitambuzinafsi ni suala ambalo limeshughulikiwa katika fasihi ya Kiswahili kiutunzi au kiutafiti. Suala hili hujitokeza kupitia kwa jinsi watunzi wa kazi za sanaa wanavyowasawiri wahusika kwa minajili ya kukuza maudhui. Usawiri wa wahusika huathiriwa na itikadi za jamii lengwa zikiwemo utamaduni hasi unaotia nguvu mfumo wa ki-ubabedume ambao umechangia pakubwa ujenzi wa ujitambuzinafsi huu. Hata hivyo, kwa kiwango fulani mwanamke mwenyewe amechangia hali hii kwa kujidunisha mwenyewe au kwa kukosa sauti na ujasiri wa kusimama kidete na kujiamulia mustakabali wake. Suala hili limejitokeza katika bunilizi za Omar Babu ambazo ni Kala Tufaha (2007), hadithi fupi ya ‘Ndoa ya Samani’ katika Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine (2010) na Heri Subira (2010). Katika bunilizi teule, mwandishi ameliangazia suala la ujenzi wa ujitambuzinafsi hasi wa jinsia ya kike kwa kiwango kikubwa. Ingawa mwandishi huyu anapania kujenga sauti ya mwanamke katika jamii iliyombana na mila zilizopitwa na wakati, katika makala hii tumelengakuonyesha na kutathmini namna ambavyo Babu amewasawiri wahusika wake ili kubainisha hali halisi ya mwanamke katika jamii husika. Uchanganuzi wetu umeongozwa na Ufeministi wa Kiafrika ambao ni mojawapo wa matapo ya Nadharia ya Ufeministi. Utamaduni unampa mwanamke nafasi gani katika jamii? Ni ipi taswira ya uhusiano wa mwanaume na mwanamke katika jamii ya Kiafrika? Je, mwanamke amechangia kwa njia gani hali yake? Tunapania kuyajibu maswali haya katika Makala haya.