Mahusiano ya Vijana wa Jinsia Tofauti katika Nathari za Kiswahili
Keywords:
Nathari, Mahusiano, Vijana, Jinsia, UsemezanoAbstract
Vijana ni wanajamii walio na umri kati ya watoto na watu wazima. Tabaka hili la wanajamii hukabiliwa na changamoto nyingi. Changamoto hizi hutokana na jaribio lao la kujitambulisha na kujiandaa kwa majukumu ya utuuzima. Changamoto hizi ni pamoja na namna ambavyo vijana wa kike hupaswa kuhusiana na wenzao wa kiume. Vijana wengi hukuza mahusiano haya, mengi yakiwa ya kimapenzi bila ya kujua namna ya kuyaendesha. Matokeo ya mahusiano haya aghalabu huwa ni kuvuruga maisha yao. Suala hili limesawiriwa na waandishi wa nathari za Kiswahili; riwaya sawa na hadithi fupi. Nathari hizi zimeitikiana na kulingana kwa kiwango kikubwa katika usawiri wa jambo hili. Ulingano huu ndio umechunguzwa katika makala haya kwa kuongozwa na nadharia ya usemezano. Makala yamebainisha kuwa kuna usemezako kati ya riwaya na hadithi fupi katika kuonyesha mahusiano ya vijana wa jinsia tofauti. Riwaya moja na hadithi mbili zimetumiwa katika makala. Riwaya ni ile ya Taswira za Mawingu(2011). Hadithi nazo ni ‘Kanda la Usufi’ kwenye diwani ya Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine (2007) na ‘Mapenzi ya Kifaurongo’ katika diwani ya Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine (2016). Makala yamechunguza ni kwa kiwango gani nathari hizi zimeshughulikia mahusiano ya vijana kwa namna inayolingana.