Usawiri wa Wanawake katika Vitabu vya Kiada vya Somo la Kiswahili katika Shule za Sekondari Nchini Kenya
Keywords:
Wanawake, Usawiri, Kiswahili, Shule za Sekondari, Vitabu vya KiadaAbstract
Makala haya yanachunguza usawiri wa wanawake katika vitabu vya kiada vya somo la Kiswahili katika shule za secondari nchini Kenya. Matini katika jumla ya vitabu vya kiada 21 yalichanganuliwa. Wilaya ya Kakamega ilitumiwa kama eneo la utafiti ili kukusanya data. Shule 33 zilitumiwa kwa lengo hili ambapo walimu wa Kiswahili 72 na wanafunzi 291 walishiriki katika uchunguzi huu. Nadharia ya kifeministi ya uhakiki wa kazi za kisanaa na ile ya uchanganuzi wa usemi zilitumiwa kuupa utafiti mwelekeo. Data iliyokusanywa ilichanganuliwa kwa kutumia programu ya tarakilishi ya SPSS. Uchunguzi huu uligundua kwa jumla kuwa vielelezo vya picha katika vitabu vya kiada viliwasawiri wanaume wengi kuliko wanawake. Vilevile wanaume wengi kuliko wanawake walitajwa. Kama ilivyotarajiwa, wanawake wengi kuliko wanaume walisawiriwa katika majukumu ya kifamilia nyumbani, huku wanaume wakisawiriwa katika ajira za kitaaluma na za hadhi ya juu kuliko wanawake. Maudhui ya vitabu hivi yaliwapendelea wanaume kuliko wanawake. Kutokana na ugunduzi huu, ilipendekezwa kuwa wakuza mitaala wahimizwe kuidhinisha vitabu vya kiada ambavyo vimejumuisha masuala ibuka kama vile jinsia na vilivyosawiri jinsia zote kwa usawa. Aidha, ilipendekezwa kuwa vitabu vitumie mifano ya wanawake waliofaulu na walionawiri katika tasnia mbalimbali kama viigwa bora kwa wanafunzi wa kike. Vilevile wanawake na wanaume wengi wenye mwamko wa kijinsia wajitose katika uwanja wa uandishi ili kuwasawiri wanawake inavyostahiki.