Mwingiliano wa Kimtindo katika Tendi
Mifano kutoka 'Mikidadi na Mayasa' na 'Kalevala'
Keywords:
Mwingilianomatini, Tendi, Mtindo, Ruwaza ya ShujaaAbstract
Uwepo wa tendi katika maeneo ya Afrika umezua mjadala na mgogoro mkali mno katika jamii ya usomi. Hii ni kutokana na rai kuwa wasomi na watafiti wengi kutoka maeneo ya Kimagharibi walidai kuwa Afrika hakuna tendi ila kinachodaiwa kuitwa tendi ni masimulizi ya kisifo tu. Wahakiki wengine wamezifutilia mbali tendi hizi kwa kudai kuwa maudhui yake ni ya kichawi na sihiri. Pia, vigezo vya kuainisha tendi vilivyotumiwa na wanazuo wa Kimagharibi vilikuwa vya kimaeneo na kimakusudi, walidhalilisha tendi za Kiafrika. Licha ya kuwa kuliibuka watafiti wa Kiafrika na kudai kuwa Kusini mwa Sahara ya Afrika kuna tendi, wao pia walielekea kutumia vigezo ambavyo ni vya kimaeneo. Ili kujaribu kutatua mzozo na utata uliopo kuhusu uwepo wa tendi katika maeneo ya Kiafrika, utafiti huu ulinuia kuchunguza iwapo kuna mwingiliano wa kimtindo baina ya tendi za maeneo haya mawili. Madhumuni makuu yalikuwa kutathmini iwapo kuna mwingiliano wa vipengele vya kimtindo baina ya tendi za Kiafrika na zile za Kimagharibi licha ya tendi za Kiafrika kufutiliwa mbali na baadhi ya wasomi wa Kimagharibi. Makala yalichunguza tendi mbili zinazopatikana katika maeneo ya Kiafrika na Kimagharibi. Tendi hizi ni Utendi wa Mikidadi na Mayasa unaopatikana Afrika na Utendi wa Kalevala unaopatikana Finland katika maeneo ya Kimagharibi.