Usawiri wa Nduni za Shujaa na Nafasi yake katika kuibua Maudhui
Ukakiki wa Kisakale cha “Mukwavinyika”
Keywords:
Shujaa, Maudhui, Kisakale, UsawiriAbstract
Mjadala wa kuwapo au kutokuwapo kwa mashujaa wa Kiafrika ulichochewa na Finnegan (1970) aliposema kuwa Afrika, Kusini mwa jangwa la Sahara hakuna tendi zinazozungumzia habari za mashujaa. Kutokana na hilo, watafiti wa Kiafrika kama vile Johnson (1978), Okpewho (1979), na Mulokozi (1999) walifanya tafiti ili kumjibu Finnegan. Matokeo ya tafiti zao yamedhihirisha kuwa, Afrika kuna tendi zinazozungumzia habari za mashujaa na ushujaa. Pia, kumhusu shujaa wa Kiafrika, watafiti hao waliorodhesha sifa kadhaa anazotakiwa kuwa nazo shujaa wa Kiafrika. Sifa hizo ni shujaa kutoka katika tabaka lolote, kusaidiwa na wahenga au mizimu, kuungwa mkono na wanajamii, kuongozwa na sihiri na kuwa na nguvu zinazojumuisha nguvu za kimwili, kiakili, kivita na urijali. Hata hivyo, imezoeleka kwa watafiti wengi kuwa mashujaa wanachambuliwa kwa kutumia utanzu wa utendi (Mtega, 2017; Kazinja, 2017 na Mulokozi, 2017). Hili, zaidi ya mengine, limesababisha hata mashujaa hao kujulikana kuwa ni mashujaa wa kiutendi. Pia, kumekuwa na tafiti chache kuhusu uchambuzi wa mashujaa wa Kiafrika kwa kutumia tanzu nyingine za fasihi kama vile visakale. Kwa kutambua hoja hiyo, makala hii inakusudia kuchunguza nduni za shujaa na nafasi yake katika kuibua maudhui huku ikidondoa mifano kutoka katika kisakale cha “Mukwavinyika.” Makala hii, imeongozwa na Nadharia ya Sifa za Shujaa wa Kiafrika na data zake zimekusanywa maktabani na uwandani. Makala hii, imebainisha kuwa, sifa za shujaa zina mchango mkubwa katika kuibua maudhui yanayosawiriwa katika visakale vya mashujaa wa jamii husika.