Ruwaza ya Viambishi vya Nafsi na Njeo katika Vitenzi vya Lugha ya Kifipa
Keywords:
Viambishi, Nafsi, Njeo, Mzizi, Ruwaza, KifipaAbstract
Makala haya yamechunguza ruwaza ya viambishi vya nafsi na njeo katika vitenzi vya lugha ya Kifipa kwa kuongozwa na Nadharia Akisi ya Baker. Data za makala haya zilipatikana kwa mbinu za hojaji na usaili ambapo vitenzi sabini na vitano (75) vya Kiswahili vilitafsiriwa kwa Kifipa na baada ya kutafsiriwa watoataarifa waliombwa wavitamke taratibu kwa Kifipa. Data zilizopatikana zilichanganuliwa kwa mkabala wa kitaamuli na kuwasilishwa kwa majedwali na vielelezo mbalimbali. Matokeo ya utafiti huu yameonesha kuwa, lugha ya Kifipa ina nafsi tatu zenye umoja na wingi. Nafsi ya kwanza umoja na nafsi ya tatu umoja huwakilishwa na viambishi viwiliviwili kwa kila nafsi. Nafsi ya kwanza wingi, nafsi ya pili umoja na wingi na nafsi ya tatu wingi huwakilishwa na kiambishi kimojakimoja kwa kila nafsi. Viambishi vyote vya nafsi hutokea kabla ya mzizi wa kitenzi. Kwa upande wa njeo, lugha ya Kifipa ina njeo tatu; wakati uliopita, uliopo na ujao. Wakati uliopita na uliopo zina viambishi bayana ilhali wakati ujao huamriwa na masuala ya kifonolojia kwa kutumia umbo la kitenzi cha wakati uliopo. Wakati uliopita una viambishi viwili vinavyotokea kwa pamoja kwenye kitenzi. Kiambishi kimoja cha wakati uliopita hutokea kabla ya mzizi na kingine hutokea baada ya mzizi wa kitenzi. Kiambishi cha wakati uliopo hutokea kabla ya mzizi wa kitenzi.