Dhana ya Utendaji na Dhima Yake katika Tamthilia ya 'Kitumbua Kimengia Mchanga'
Keywords:
Utendaji, Tamthilia, Nadharia ya Utendaji, Drama, Vipengele vya UtendajiAbstract
Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya utendaji iliyoasisiwa na Wallace Bacon ili kubainisha ikiwa tamthilia ya Kitumbua Kimeingia Mchanga iliyoandikwa na Mohamed (2000) imezingatia kigezo kikuu katika matini za kidrama ambacho ni uwezo wa kuwasilishwa jukwaani au ni majibizano ya usemi tu. Katika utafiti huu tumevitathmini vipengele vinavyochochea na kufanikisha utendaji wa tamthilia kwenye jukwaa. Maelekezo ya jukwaa, mandhari, maleba, miondoko, sauti, uangazaji, kimya na mihimili ni vipengele vya utendaji ambavyo huwawezesha waigizaji kuwasilisha ujumbe wa mwandishi kwenye jukwaa. Utafiti huu umejaribu kubainisha jinsi vipengele hivi vinavyofanikisha uwasilishaji wa ujumbe kwenye jukwaa na pia kutaja kwa ufupi dhima zinazofungamana na matumizi ya vipengele hivi. Utafiti huu ulihusisha kusoma makala na kutumiwa kama data ya utafiti huu ambayo baadaye ilichanganuliwa na mwishowe kuelezea matokeo kwa kutumia mbinu ya kimaelezo. Utafiti huu pia ulihusisha ukusanyaji wa data moja kwa moja kutoka maktabani. Mahali pa utafiti palikuwa ni maktaba katika vyuo vikuu pamoja na maktaba ya kitaifa nchini Kenya na kundi lengwa lilikuwa tamthilia ya Kitumbua Kimeingia Mchanga. Inatarajiwa kuwa utafiti huu utakuwa mchango mkubwa kwa jamii ya wasomi hasa wanaoshughulikia utendaji na vipengele vya kidrama katika fasihi andishi.