Uchanganuzi wa Sitiari za Bahari katika Methali za Waswahili
Keywords:
Methali, Sitiari, Bahari, Mawanda Chanzi, Mawanda Lengwa, WaswahiliAbstract
Makala hii inachanganua sitiari za bahari katika methali za Waswahili. Methali ni mojawapo ya vipera vya fasihi simulizi. Kufuatia ujio wa maandishi na teknolojia, vipera vingi vya fasihi simulizi vilianza kutiwa katika maandishi na kuwa fasihi andishi pia. Kwa mujibu wa Simiyu (2011), ni semi fupi zinazosheheni mafumbo juu ya ukweli wa maisha ya binadamu, naye Mieder (2014) anasema sifa kuu za methali ni ufupi wake, uthabiti na uasili. Fasihi simulizi ya kila jamii huakisi mazingira, utamaduni na mwono-ulimwengu wao. Katika fasihi simulizi zao, mila, desturi na maadili yao pia hujitokeza. Mazingira ya Waswahili yana mchango mkubwa katika kuumba fasihi simulizi yao, methali zikiwemo. Mazingira ya minazi, bahari, vyombo vya bahari, samaki, visima na vitu vingine vinavyopatikana katika mazingira ya Waswahili ndivyo huumba methali zao. Vitu hivi hutumiwa kistiari katika methali zao na kupanua maana za vitu hivyo kifasihi. Makala hii inachanganua sitiari za bahari ambayo ni sehemu mojawapo ya mazingira ya Waswahili.