Maumbo ya Fasihi Simulizi katika Mashairi Andishi Teule ya Kiswahili
Keywords:
Fasihi Simulizi, Mashairi, MaumboAbstract
Asili ya mashairi ya Kiswahili ni nyimbo simulizi za jamii za Afrika mashariki. Pamoja na vipera vingine vya fasihi simulizi, nyimbo huingiliana katika kujenga mashairi andishi ya Kiswahili. Hata hivyo baadhi ya wasomi katika viwango anuwai wamepuuza fasihi simulizi na kuichukulia kama utanzu sahili wenye thamani duni huku ushairi ukidhukuriwa kama utanzu tata. Makala hii inatalii maumbo ya fasihi simulizi katika mashairi andishi ya Kiswahili ili kuonyesha thamani ya fasihi simulizi katika kujenga mashairi andishi. Data sekondari ilikusanywa kwa kudurusu diwani tatu zilizoteuliwa kimaksudi kuwakilisha vipindi vitatu katika historia ya ushairi mathalani Utenzi wa Fumo Liyongo (Kijumwa, 1964) kuwakilisha kipindi cha urasimi, diwani ya Sauti ya dhiki (Abdalla, 1973) kuwakilisha kipindi cha urasimi mpya na diwani ya Kichomi (Kezilahabi, 1974) katika awamu ya sasa. Data iliyokusanywa ilichanganuliwa kwa mtindo wa uchanganuzi wa matini. Uchunguzi ulionyesha kuwa maumbo manne makuu ya fasihi simulizi hujenga mashairi andishi ya Kiswahili. Matokeo haya ni muhimu kwa kuonyesha nafasi ya fasihi simulizi katika mashairi andishi na hivyo kuonyesha namna fasihi simulizi inavyoweza kutumika kusahilisha uchambuzi wa mashairi.