Kapitalosenia kama Pantoni ya Anthroposenia katika Riwaya ya Kiswahili
Mfano wa 'Vipuli vya Figo', 'Mafuta' na 'Walenisi'
Keywords:
Anthroposenia, Kapitalosenia, Pantoni, Uhakikimazingira, Ubepari, UwezoAbstract
Makala haya yanashughulikia kapitalosenia kama pantoni ya anthroposenia katika nchi za Afrika katika riwaya ya Emmanuel Mbogo: Vipuli vya Figo; na za Katama Mkangi: Mafuta na Walenisi. Riwaya hizi tatu zilisomwa na mtafiti na hatimaye data iliyodhihirisha kapitalosenia kama pantoni ya anthroposenia ilitongolewa mintarafu ya lengo la makala haya. Kusudi kuu la makala haya lilikuwa kujadili namna kapitalosenia huvusha anthroposenia kutoka mataifa ya ughaibuni hadi barani Afrika katika riwaya nne teule za Kiswahili katika misingi ya kiuhakikimazingira. Baadhi ya nguzo kuu za nadharia ya uhakikimazingira, kama vile; uongozi mbaya, kifo na uwezo, utamaduni na mazingira, na utandawazi, ziliongoza uhakiki wa makala haya, mintarafu ya lengo la makala. Sababu kuu ya kuhakiki riwaya hizi ilikuwa kukidhia data ya tahakiki zinazohusu mchango wa kapitalosenia katika anthroposenia barani Afrika katika riwaya ya Kiswahili. Ilidhihirika kwamba, kando na mataifa yenye uwezo kuyanyonya yale fukara ya Afrika rasilimali asilia, taaluma, wataalamu, na watumwa kama wafanyakazi madhubuti, yanapujua mazingira ya Afrika bure na kwa hiari yao wenyewe. Ingawa unajisi huu wa kimazingira unaathiri utamaduni na jamii kwa jumla, chumi za Afrika zilidhihirisha udhoofu wa hali ya juu kutokana na kiwango cha ufukara unaokita mizizi katika nchi za Afrika.