Tathmini ya Binadamu na Mazingira katika Riwaya ya 'Nakuruto'
Keywords:
Binadamu, Mazingira, Uhakikimazingira, Maadili ya Mazingira, MaumbileAbstract
Makala haya yalinuia kudhihirisha jinsi binadamu huingiliana na mazingira yake katika riwaya ya Nakuruto ya mwandishi maarufu – Clara Momanyi – na mwenye mwelekeo chanya dhidi ya mazingira kama inavyodhihirika katika matini yake. Uhakiki huu uliongozwa na baadhi ya nguzo kuu za nadharia ya uhakikimazingira, kama vile, utamaduni na maumbile, binadamu dhidi ya maumbile, maadili ya mazingira, baina ya zingine kadhaa. Momanyi aliandika matini ya Nakuruto wakati ambapo kazi za fasihi ya kimazingira zilikuwa haba. Binadamu katika shughuli zake za kila siku, huweza aidha kuyatunza au kuyachafua mazingira. Mara nyingi ni uchafuzi ambao hutekezwa zaidi kuliko uhifadhi. Hili lilidhihirishwa na tathmini hii, ambapo ilibainika kuwa mwanadamu amekuwa akiyapuuza mazingira, lakini jinsi muda unavyosonga mbele ndivyo ameanza kumakinikia na kuajibikia mazingira. Uajibikaji huu umeimarisha uhifadhi wa mazingira kama inavyodhihirika katika riwaya ya Nakuruto.Uhakikimazingira ni usomi wa fasihi na mazingira kwa kujikita katika mwelekeo unaohusu maeneo ya taaluma zaidi ya moja. Hivyo, kwa msingi huu, makala haya yaliafikia kutathmini matini ya Nakuruto ambayo ina masuala ya kimazingira na kujaribu kumaizi jinsi ambavyo Momanyi amedhihirisha mchango wa binadamu katika mazingira kisanaa.