Uchunguzi wa Kidrama wa Riwaya ya Kiswahili na Maendeleo ya Fasihi Afrika Mashariki
'Unaitwa Nani?' ya K.W. Wamitila
Keywords:
Drama, Dayalojia, Riwaya, Usemezano, 'Jarabati'Abstract
Katika makala haya ninachunguza namna dayalojia ya kidrama inavyotumika katika riwaya za kisasa za Kiswahili kama mbinu mojawapo ya kuwasilisha fikra na mawazo katika kazi ya fasihi; mintarafu riwaya ya Unaitwa nani? ya Wamitila. Baadhi ya riwaya za Kiswahili hasa zile zilizoandikwa mwishoni mwa karne ya 20 na mwanzoni mwa karne ya 21 zimekuwa zikitumia fani mbalimbali za kiusasa-baadaye katika fasihi jarabati, msisitizo ukiwa kwenye matumizi ya fantasia ili kuwasilisha ujumbe. Katika uchunguzi huu nimejikita katika riwaya ya Unaitwa nani? nikitathmini matumizi ya fani ya dayalojia au lugha ya majibizano kama ilivyotumika katika riwaya kwa minajili ya kuwasilisha fikra. Nimetathmini lugha ya majibizano na usemezano kama inavyobainika katika Unaitwa nani Mijadala mbalimbali inayojitokeza na inavyoendelezwa kuhusiana na suala la kijinsia imezingatiwa kwa makini. Hatimaye kazi hii imekadiria mchango wa riwaya za kiusasa - baadaye katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kwa jumla na hususan katika ukanda wa Mashariki mwa Afrika. Uchunguzi huu umeongozwa na nadharia ya usemezano ya Mikhail Bakhtin.