Nafasi ya Kiswahili katika Utoaji wa Huduma za Afya Tanzania
Keywords:
Huduma za Afya, Kiswahili, TanzaniaAbstract
Lugha ya Kiswahili kama zilivyo lugha nyingine duniani, hufanikisha mawasiliano katika jamii. Mawasiliano hayo yanaweza kuwa ya watu wa utamaduni mmoja au watu wa jumuiya kubwa zenye wazungumzaji wa lugha mbalimbali na wenye tamaduni tofauti. Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na jamii kubwa zaidi Afrika Mashariki hususan Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Kongo na kwingineko (Kiango, 2002). Lengo la makala haya si kujadili nafasi ya Kiswahili kwa mwelekeo wa mawanda hayo mapana, bali kujielekeza katika eneo mahususi ili kubainisha na kujadili nafasi ya Kiswahili katika utoaji wa huduma za afya nchini Tanzania. Makala haya yanazingatia kuwa licha ya lugha ya Kiswahili kuwa lugha inayofahamika sana kwa Watanzania waliowengi, zipo changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania wanapotumia lugha ya Kiswahili wakati wa kutoa au kupokea huduma za afya nchini. Changamoto hizi ni pamoja na wataalamu wa afya kupata mafunzo kwa lugha za kigeni suala linalosababisha wataalamu hao kukosa msamiati wa kitaalamu wa lugha ya Kiswahili, matumizi ya lahaja mbalimbali za Kiswahili, kutofautiana kwa lugha mama na tamaduni za lugha husika na matumizi ya misimu au lugha za mitaani. Kutokana na changamoto hizi, lugha ya Kiswahili hushindwa kutumika kikamilifu katika mawasiliano baina ya watoaji na wapokeaji wa huduma za afya.