Tofauti ya Kimiundo kati ya Vivumishi na Vibainishi katika Lugha ya Kiswahili kwa Mtazamo wa Eksibaa
Keywords:
Vivumishi, Eksibaa, Vibainishi, Kiswahili, SintaksiaAbstract
Pamoja na wanasarufi wa lugha ya Kiswahili kukubaliana kuwapo kwa uainishaji wa vivumishi na vibainishi lakini kwa kiasi kikubwa, ukipitia kazi za wataalamu mbalimbali, dhana hizo zimekuwa zikichanganywa katika kapu moja la uainishaji katika lugha ya Kiswahili. Kwa mantiki hiyo, maneno ya vivumishi yameanishwa kama vibainishi na vibainishi kuainishwa kama vivumishi. Hivyo uainishaji wa vivumishi na vibainishi katika lugha ya Kiswahili umekuwa na dosari hasa katika uingizaji wa mifano ya maneno katika kategoria hizo. Maneno yaliyoelezwa kama vibainishi na wataalamu kama; Habwe na Karanja, (2004), Biber na wenzake (2005), Richards na wenzake (2010), Khamis (2011). Pia yameelezwa kama vivumishi na wataalamu wengine au wataalamu walewale. Maneno ya aina moja kutumika katika kategoria mbili tofauti, kumeleta ukinzani wa kiuchanganuzi hasa katika sintaksia ya lugha ya Kiswahili. Makala haya yamekusudia kubainisha tofauti ya kimiundo kati ya vivumishi na vibainishi kwa mtazamo wa Eksibaa, ili kuweka wazi tofauti kati ya vibainishi na vivumishi na kufanya uainishaji wa kategoria mbili hizi, kutoingiliana kama inavyojitokeza katika kazi za wataalamu. Makala haya yameweka wazi mwachano kati ya vivumishi na vibainishi kama kategoria mbili tofauti katika lugha ya Kiswahili.