Ulinganishi wa Kiisimu wa Lugha za Kiswahili na Kiarabu
Keywords:
Kiswahili, Kiarabu, Isimu, Fonolojia, Mofolojia, Sintaksia, Mfumo wa NgeliAbstract
Makala haya yanalinganisha vipengele vya kiisimu baina ya lugha za Kiswahili na Kiarabu ili kubaini iwapo lugha hizi zina asili moja au la. Itakumbukwa kwamba mnamo mwanzoni mwa miaka ya 1970 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam palijitokeza mijadala iliyozusha mabishano na malumbano ya kitaaluma kuhusu asili na chimbuko la lugha ya Kiswahili. Kuna waliodai kuwa lugha ya Kiswahili ilitokana na lugha ya Kiarabu na wengine wakaeleza kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu (Massamba, 2007). Ushahidi wa kila upande uwe na mashiko au usiwe na mashiko ulitolewa, lakini ulinganishi wa kiisimu wa lugha hizi bado haujafanyika. Kwa sababu hiyo ndipo tukaamua kulinganisha isimu ya lugha mbili hizi. Data ya uchunguzi huu imekusanywa kutoka maktabani ambapo mwandishi amepitia maandiko na machapisho mbalimbali yanayohusiana na kazi hii. Matokeo ya uchunguzi huu yanabainisha kuwa lugha ya Kiswahili haitokani na Kiarabu. Kwa sababu katika vipengele vitano vya kiisimu tulivyovilinganisha katika makala haya, vyote vinaonesha kuwa lugha hizi zinatofautiana kiisimu. Vipengele vilivyolinganishwa ni msamiati wa msingi, fonolojia, mofolojia, sintaksia na mfumo wa ngeli. Kutokana na tofauti hizo tunaweza kuhitimisha kuwa lugha hizi hazina asili wala mnasaba mmoja.