Dhima za Uradidi katika Mawasiliano ya Kihaya
Keywords:
Uradidi, Umboghafi, Umbotokeo, Kudunisha Maana, Kuimarisha MaanaAbstract
Makala hii inachunguza dhima za uradidi katika mawasiliano ya Kihaya. Eneo ambalo data ya makala hii imepatikana ni kata ya Mayondwe katika wilaya ya Muleba mkoani Kagera. Data ya makala hii imepatikana kwa kutumia mbinu mbili; mbinu ya mahojiano na ya maktabani. Mbinu ya mahojiano imehusisha majibizano baina ya pande mbili, yaani mtafiti na watafitiwa. Lengo la mbinu ya mahojiano ni kupata taarifa zinazohusiana na mada ya makala yetu. Aidha, uteuzi wa mbinu hii ulizingatia ukweli kwamba, mbinu hii husaidia kupata taarifa za ziada ambazo si rahisi kuzipata kwa kutumia mbinu nyingine za ukusanyaji data. Mtafiti aliitumia mbinu ya maktabanikwa kusoma vitabu na makala mbalimbali katika maktaba ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kupata maarifa yanayohusiana na mada ya makala yetu. Halikadhalika, sampuli ya watafitiwa 10 ambao ni wazawa wa mkoa wa Kagera na wazungumzaji wa lugha ya Kihaya ndiyo waliotumika katika makala hii. Vijana walikuwa 5 na watu wazima 5. Data iliyokusanywa imechambuliwa kwa kutumia nadharia ya Uelekeani iliyoasisiwa na McCarthy na Prince (1993, 1994a, 1994b na 1995). Matokeo ya makala hii yanaonesha kuwa uradidi katika lugha ya Kihaya una dhima kadhaa. Mathalani, kufanyika vibaya kwa tendo au ukosefu wa umakini, kufanyika mara kwa mara kwa tendo husika, uharaka wa tendo husika, kudunisha maana, kuongeza msisitizo pamoja na kubadili maana. Inapendekezwa kuwa, tafiti zaidi zifanyike kuhusiana na dhana ya uradidi kwa ujumla. Mathalani, ujitokezaji wa uradidi katika Kihaya kwa kuangazia kategoria za nomino, vielezi, vivumishi, vitenzi nakadhalika. Aidha, utafiti ufanyike kuhusiana na dhima za uradidi katika lugha mbalimbali kama vile: Kiswahili, Kisukuma, Kichaga na lugha nyinginezo.