Ujitokezaji wa Viambishi vya Nafsi katika Kiarabu, Kitumbatu na Kiswahili
Keywords:
Viambishi, Kategoria, Mapisi, Kusigana, Hayajatindimaa, MuasalaAbstract
Makala haya yanalenga kuchunguza ujitokezaji wa viambishi vya nafsi katika Kiarabu Kitumbatu na kuvilinganisha na Kiswahili. Lengo la uchunguzi huo ni kutaka kubaini jinsi vipengele hivyo vinavyoingiliana na kusigana. Hii inatokana na ukweli kwamba mapisi ya lugha ya Kiswahili na lahaja zake pamoja na lugha ya Kiarabu mpaka sasa hayajatindimaa kwa kuwa lugha hizi zilikuwa na mtagusano na muasala wa muda mrefu tangu 800 BK. Kutokana na hali hiyo, kumeibuka mitazamo kinzani juu ya uhusiano wa Kiswahili na Kiarabu. Kuwapo kwa baadhi ya maneno ya Kiarabu katika Kiswahili kumechochea hoja kwamba Kiswahili kinatokana na Kiarabu. Mjadala huo ni wa muda mrefu ambao unaendelea hadi sasa. Baadhi ya tafiti tangulizi zimebainisha idadi kubwa ya maneno ya Kiswahili yenye asili ya Kiarabu. Hata hivyo, mfanano huo wa kimsamiati baina ya Kiswahili na Kiarabu haujitoshelezi kutoa hitimisho juu ya chimbuko la Kiswahili. Baadhi ya watafiti waliochunguza maneno ya Kiarabu katika Kiswahili wamebaini kuwapo kwa asilimia kubwa ya mfanano wa kategoria ya nomino baina ya lugha hizi mbili kuliko katika kategoria zingine. Hivyo, pamoja na kuwapo kwa kategoria mbalimbali za maneno, utafiti huu umejibana kushughulikia jinsi viambishi vya nafsi vinavyojitokeza katika kategoria ya vitenzi vya Kiarabu, Kitumbatu na kuvilinganisha na Kiswahili. Hii ni kwa sababu kwa kuwa imeshatibitika kwamba, Kitumbatu ni miongoni mwa lahaja ya Kiswahili, ujitokezaji huo wa viambishi utatupa mwanga kati ya uhusiano wa Kiarabu na Kiswahili. Chanzo cha data za utafiti huu zimekusanywa kupitia usomaji wa nyaraka, vitabu na kamusi mbalimbali zilizoandikwa kuhusu kategoria hiyo. Vilevile, tulipitia nyaraka hizo ili kupata maarifa ya jumla kuhusu ujitokezaji wa viambishi vya nafsi kwa mujibu wa waandishi mbalimbali. Data zingine zilikusanywa uwandani kupitia mbinu ya usaili na hojaji kwa wazungumzaji wa Kiarabu na Kitumbatu. Aidha, utafiti huu umeongozwa na Nadharia ya Fonolojia Umbo Upeo kuanzia sasa (UU). Kwa ujumla matokeo ya utafiti huu yameonesha kwamba Kitumbatu kina uhusiano zaidi na Kiswahili kuliko Kiarabu. Hii ni kudhihirisha kwamba Kiswahili na Kiarabu ni lugha mbili ambazo hazina uhusiano wa kimnasaba kwa kuwa hazikuchipukia kutoka kwenye lugha yenye asili moja.