Dhima za Vibainishi Vioneshi katika Kiswahili Sanifu
Keywords:
Vibainishi, Vioneshi, Kiswahili, MofolojiaAbstract
Makala haya yamechunguza vibainishi vioneshi katika lugha ya Kiswahili ili kubaini dhima za vibainishi hivyo. Lengo hasa likiwa ni kudhukuru dhima za vibainishi vioneshi ambapo mara nyingi wataalam huelezea dhima moja ya vibainishi ambayo ni kuonesha masafa ya ukaribu au umbali. Data za makala haya yalikusanywa maktabani kutoka katika matini za vitabu vya Kichwamaji (Kezilahabi, 1974) na Kivuli Kinaishi (Mohamed, 1990). Mbinu iliyotumika ni usomaji wa maandiko na kunukuu madondoo yanayohusiana na dhima za vibainishi vioneshi. Data hizo zilichambuliwa kwa mbinu ya maelezo. Nadharia ya Mofolojia Leksika iliyoasisiwa na Kiparsky (1982) ilitumika. Kwa muhtasari, matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kwamba vibainishi vioneshi vina dhima mbalimbali ikiwa ni pamoja na dhima ya kuonesha mahali, dhima ya kuhimiza, msisitizo, kuunganisha na kuonesha umbali au ukaribu wa kitu. Makala haya yanapendekeza kwamba, utafiti mwingine ufanyike katika aina zingine za vibainishi ili kupata maarifa majumui kuhusu dhima za vibainishi hivyo katika lugha ya Kiswahili. Pia, utafiti unaweza kufanywa kuchunguza dhima za vibainishi katika lugha mbalimbali za Kibantu ili kuona namna dhima zinavyoweza kutofautiana na/au kufanana na zile za lugha ya Kiswahili.