Uchanganuzi wa Mkazo katika Maneno ya Kiswahili Sanifu
Keywords:
Mkazo, Silabi, Nguvumsikiko, Fonolojia, KiswahiliAbstract
Makala haya yamechukuza udhihirikaji wa mkazo katika maneno ya Kiswahili Sanifu ili kuweza kubaini utokeaji wa mkazo katika neno. Lengo hasa ilikuwa kuchunguza namna mkazo unavyojibainisha katika neno. Utafiti huu ulilenga kuchunguza mkazo katika Kiswahili sanifu. Hii inatokana na namna mkazo unavyojitokeza kwa kuonesha msigano wa nguvumsikiko baina ya viambajengo vinavyohusika katika neno yaani silabi. Uchunguzi huu unashadidiwa na uchanganuzi wa mkazo kinadharia kuwa kila kiambajengo kina nguvumsikiko fulani ambayo husababisha kuwepo na aina za mkazo. Data zilikusanywa uwandani kwa njia ya mahojiano na ushuhudiaji. Mbinu zilizotumika katika uchanganuzi wa data ni mkabala wa kimaelezo na kiidadi. Nadharia ya Fonolojia Mizani (FM) imetumika katika uchanganuzi wa data. Data zimewasilishwa na kufanyiwa uchanganuzi kwa kutumia mifano, vielelezo, michoro na ufafanuzi. Matokeo yanaonesha kuwa mkazo uliokuwa unashughulikiwa katika tafiti zilizotangulia ni mkazo msingi tu, bila kuhusisha mkazo katika silabi nyingine ambazo zinapotamkwa huwa na nguvumsikiko fulani wakati wa utamkaji. Kwa mantiki hiyo silabi nyingine nazo zina mkazo. Hivyo, kuweza kuwa na mkazo upili, utatu na kadhalika kutegemea na viambajengo katika neno husika. Aidha, utokeaji wa mkazo katika viwango tofauti tofauti kati ya silabi zinazounda neno husika imetudhihirishia kuwa kiuchanganuzi katika Kiswahili sanifu kuna aina za mkazo kutegemeana na kiwango cha nguvumsikiko.