Mifanyiko ya Kimofofonolojia ya Konsonanti za Nomino Mkopo za Kiturkana kutoka Kiswahili
Keywords:
Nomino Mkopo, Udhoofikaji, Uimarikaji, Uchopekaji, Usilimisho Pamwe wa Nazali, UbadalaAbstract
Makala haya yanahusu mifanyiko ya kimofofonolojia ya konsonanti za nomino mkopo za Kiturkana kutoka Kiswahili. Uchunguzi huu ulikusudia kuchunguza mabadiliko yanayokumba konsonanti za nomino za Kiswahili zinapokopwa na Kiturkana. Nadharia ya fonolojia zalishi asilia ilielekeza uchunguzi wetu katika kubaini mifanyiko ya kimofofonolojia ambayo konsonanti za nomino mkopo za Kiturkana kutoka Kiswahili hupitia na kanuni zinazodhibiti mifanyiko hii. Tulikusanya data yetu maktabani yaani kutoka kwa Bibilia ya Kiturkana, Misali na Kamusi ya Kiingereza — Kiturkana na kuwasilisha kifonetiki na kiothografia. Utafiti huu umebaini kwamba kuna fonimu ambazo zipo katika Kiswahili lakini hazipo katika Kiturkana. Uchunguzi wetu umetambua kwamba konsonanti za Kiswahili zinapokopwa na Kiturkana hupitia mabadiliko ya kifonolojia kama vile udhoofikaji, uimarikaji, udondoshaji, uchopekaji, usilimisho pamwe wa nazali na ubadala wa konsonanti ili nomino hizi zikubalike katika Kiturkana kwa lengo la kusahilisha utamkaji, kupata muundo mwafaka wa silabi na mofu ya jinsia ambayo hutumiwa kuainisha nomino za Kiturkana.