Ukamilifu na Utimilifu wa Kifasihi katika Maandishi ya Kubuni
Mfano wa Riwaya Teule za Said Ahmed Mohamed
Keywords:
Muwala, Ukamilifu, Utimilifu, Viambajengo, Fani, Maandishi ya KubuniAbstract
Makala haya yanalenga kuhakiki muwala au mshikamano wa viambajengo vya fani katika riwaya teule za Said Ahmed Mohamed: Dunia Mti Mkavu (1980) na Kiza Katika Nuru (1988). Uhakiki huu unahusisha viambajengo vinne tu vya fani: wahusika, msuko, mandhari na mtindo. Lengo kuu la uhakiki huu ni kuonyesha ni kwa vipi muwala au muumano wa vipengele vya fani unachangia kudhihirisha ukamilifu na utimilifu wa kifasihi katika kazi ya sanaa kupitia riwaya hizi. Kwa kufanya hivyo, mhakiki anachunguza iwapo riwaya hizi zinadhihirisha muwala wa vipengele vya msuko, usawiri wa wahusika, mandhari na mtindo, hivyo kumwezesha kufikia maamuzi iwapo riwaya husika zimefikia ukamilifu na utimilifu wa kifasihi. Matokeo ya utafiti huu ni kuwa ili kazi ya ubunaji idhihirishe ukamilifu na utimilifu wa kifasihi, ni sharti viambajengo vya fani vidhihirishe muwala au muumano. Katika mkabala huu, makala hii inadadavua jinsi riwaya ya Dunia Mti Mkavu (1980) inavyokosa muwala ikilinganishwa na riwaya ya Kiza Katika Nuru (1988), hivyo umaarufu wake kutopata uhai kifani kwa kiasi fulani, tofauti na vile Mazrui (1984) anavyogundua kwa upande wa maudhui. Halikadhalika, matokeo ya uhakiki huu yamedhihirisha kuwa, mpangilio dhoofu wa matukio kiwakati, unaathiri uumbaji wa wahusika na msuko wa matukio katika riwaya ya Dunia Mti Mkavu (1980) hali inayoinyima ukamilifu na utimilifu wa kifasihi kwa kiwango fulani, tofauti na riwaya ya Kiza Katika Nuru (1988).