Mielekeo ya Watoaji na Wapokeaji wa Huduma za Afya kuhusu Matumizi ya Kiswahili katika Uga wa Afya Mkoani Dodoma
Keywords:
Mielekeo, Madaktari, Wahudumu wa Mapokezi, Wagonjwa, WajawazitoAbstract
Makala haya yanalenga kuchunguza mielekeo ya watoaji na wapokeaji wa huduma za afya kuhusu matumizi ya Kiswahili katika huduma za afya. Data ilikusanywa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya nne za mkoa wa Dodoma nchini Tanzania ambazo ni: Bahi, Kongwa, Chamwino na Dodoma. Data zimechanganuliwa kwa kuongozwa na Nadharia ya Vitendo Vilivyofikiriwa ya Azjen na Fishbein ya Mwaka 1980. Matokeo ya utafiti yamedhihirisha kwamba watoaji na wapokeaji wa huduma za afya ambao ni madaktari, wahudumu wa mapokezi, wagonjwa pamoja na wajawazito wana mielekeo chanya na hasi kuhusu matumizi ya Kiswahili katika huduma za afya. Mielekeo chanya ya juu kabisa ni 98.86% kwa kategoria ya wajawazito na mielekeo hasi ya juu kabisa ni 26.4% kwa madaktari. Kwa ujumla, kiwango cha chini kabisa cha mielekeo chanya na kiwango cha juu kabisa cha mielekeo hasi vyote vilidhihirika kwa madaktari. Sababu za mielekeo chanya ni pamoja na kuwa Kiswahili ni lugha ya taifa, hivyo, inaelekea kuwa na watumiaji wengi wa lugha. Baadhi ya sababu za mielekeo hasi ni pamoja na kasumba za wasomi kudharau Kiswahili. Makala haya yanapendekeza kuwa mchakato wa kubadili mielekeo ya lugha hasa kwa madaktari ufanywe kwa masilahi mapana ya watumiaji wa huduma za afya.