Itikadi za Ujinsia katika Maumbo ya Majina ya Kikuria
Keywords:
Itikadi za Ujinsia, Maumbo, Majina, Shughuli, WakuriaAbstract
Majina ni vipengele vya lugha ambavyo hutaja mtu, kitu, hali, mahali, dhana na tendo na huweza kufunua itikadi na matukio katika maisha ya wanajamii. Itikadi ni mawazo ambayo humwongoza kila mtu ulimwenguni katika kutenda anayotenda na hivyo kuhalalisha au kuharamisha matendo anayoyafanya. Makala haya yanajikita katika kuchanganua jinsi maumbo ya majina ya Kikuria katika jamii ya Wakuria iliyoko nchini Kenya hushamirisha itikadi za ujinsia. Itikadi za ujinsia ni imani, mielekeo na mitazamo inayoongoza jamii kuhusu mgawanyo wa majukumu kwa kuangalia jinsia. Lengo kuu la makala haya ni kuainisha jinsi maumbo ya majina ya Kikuria hudumisha na kuendeleza itikadi za ujinsia. Data iliyotumika katika makala haya ilikusanywa kwa njia ya mahojiano ya ana kwa ana na majadiliano ya makundi. Ukusanyaji na uchanganuzi wa data uliongozwa na Nadharia ya Onomastiki. Nadharia hii imekuwa dira katika kubainisha maumbo ya majina ya Wakuria na jinsi maumbo haya huakisi itikadi za ujinsia katika jamii ya Wakuria. Utafiti wetu uliweza kubainisha kuwa vipo vipashio ambavyo hudokeza jinsia na shughuli inayohusishwa nazo au nafasi yake katika jamii. Kwa misingi hii, utafiti wetu ulibainisha kuwa jinsia ya kiume kwa mujibu wa majina yao yaliyoteuliwa kiitikadi, ilitengewa shughuli na nafasi zilizoikweza ikilinganishwa na jinsia ya kike.