Muakiso wa Uhalisi wa Kauli za Mhusika Mlevi na Uchagizaji wa Tafsiri kwa Msomaji katika Fasihi ya Kiswahili
Keywords:
Uhalisi, Tafsiri, Fasihi, KiswahiliAbstract
Tamthiliya ya Kiswahili ni miongoni mwa kazi za kisanaa zenye wajibu mkubwa wa kuijenga jamii katika hali mbalimbali kupitia wahusika wake. Kwa kawaida, wahusika hudhibitiwa na kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na muktadha wa utunzi, hasa mawazo yanayowahusu waandishi kulingana na falsafa zao, mazingira yao, utamaduni wao, hali yao ya maisha na harakati zilizopo katika jamii inayohusika. Kwa msingi huo, makala haya yanachunguza muakiso wa uhalisi wa kauli za mhusika mlevi na jinsi zinavyochagiza tafsiri kwa msomaji. Imefanya hivyo kwa kurejelea tamthiliya teule za Lina Ubani (1984) na Mabepari wa Bongo (2007). Uchunguzi ulikuwa wa maktabani uliohusisha uhakiki wa tamthiliya zilizolengwa. Data zilikusanywa katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha kilichopo mkoani Iringa kwa kudurusu kazi mbalimbali zilizohusiana na mada iliyochunguzwa. Uchambuzi na mjadala wa data zilizowasilishwa umeongozwa na nadharia ya Ucheshi. Makala haya yanahitimisha kwamba, mhusika mlevi ni mojawapo ya mawakala wa kazi za kifasihi kwa kuwa huyafichua na kuyaweka wazi yale yote yanayoshindikana kusemwa na wahusika wanaoongea na kutenda wakiwa katika ung’amuzi tambuzi.