Athari ya Ukiushi wa Kisarufi katika Tafsiri ya Matini katika Majukwaa ya Kidijiti
Keywords:
Athari, Ukiushi, Tafsiri, SarufiAbstract
Jukumu la kimsingi la lugha kama mfumo wa maana unaowakilishwa kwa maumbo ya kisarufi ni kukidhi mahitaji ya mawasiliano miongoni mwa watumiaji wake. Lugha hupata uamilifu huu pale vipashio vyake vinapopangwa kulingana na kanuni za kimofosintaksia za lugha hiyo. Mpangilio huu ndio unaozalisha matini zenye mshikamano na ambazo hujitosheleza kimaana. Hata hivyo, dhima hii inaweza kuvurugwa pale ambapo maana inayowasilishwa katika lugha fulani imefumwa kutokana na tafsiri. Japo matini chanzi inatarajiwa kuchakatwa kwa usadifu katika matini lengwa, kadhia ya tafsiri na tofauti kati ya lugha chanzi na lugha lengwa huweza kufisidi maana. Hali hii huelekea kudhihirika zaidi kutokana na maendeleo ya Tehama ambayo yameathiri pakubwa matumizi ya lugha ikiwemo taaluma ya tafsiri. Ni kutokana na hoja hii ambapo makala haya yanaangazia jinsi ukiushi wa kisarufi unavyoathiri maana ya matini tafsiri katika Majukwaa ya Kidijiti. Uteuzi wa kimakusudi ulitumiwa ili kupata sampuli sadifu ya data kutoka tuko.com na bbc.com. Data zilizokusanywa na zilichanganuliwa kinathari huku majedwali yakitumiwa kuweka wazi matokeo. Matokeo ya utafiti huu yanatazamiwa kuwa na umuhimu wa kutoa maarifa kuhusu mbinu na mikakati ya uhawilishaji waujumbe wenye muumano kwa watafsiri wa matini asilia na za mtandaoni. Waaidha, kazi hii itanufaishamashirika ya uanahabari na wanahabari huria wanaonuia kuboresha tafsiri za taarifa zao na vilevile kuchochea wasomi wanaonuia kutafiti kuhusu masuala ya kipragmatiki yanayodhihirika katika tafsiri za lugha mbalimbali.