Uchanganuzi wa Makosa ya Kitahajia katika Mawasiliano Andishi ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu
Mifano kutoka Chuo Kikuu cha St John’s cha Tanzania
Keywords:
Makosa ya Tahajia, Mawasiliano, Wanafunzi, Vyuo VikuuAbstract
Maandishi ya wanafunzi ni njia muhimu ya kuwasilisha hoja zao chuoni hususan katika masuala yanayohusiana na utahini. Utokeaji wa makosa katika kazi za wanafunzi ni jambo ambalo hupelekea kuvurugika kwa mawasiliano na wakati mwingine hata huwafanya wapate alama za chini wanapotahiniwa. Ingawa kuna tafiti nyingi ambazo zimefanywa kuhusu utokeaji wa makosa katika maandishi ya wanafunzi, makosa katika maandishi ya wanafunzi wa vyuo vikuu hayajaangaziwa sana. Ni kutokana na hali hii ambapo makala haya yanalenga kutambulisha na kuainisha makosa ya kitahajia yanayojitokeza katika mawasiliano andishi ya wanafunzi wa vyuo vikuu na kupendekeza mbinu zinazoweza kutumiwa ili kupunguza utokeaji wake. Data imekusanywa kutokana na mawasiliano andishi ya wanafunzi katika mawasilisho ya semina na mijarabu ya darasani. Wanafunzi waliohusishwa kama watafitiwa ni wa mwaka wa kwanza, wa pili na wa tatu. Uchanganuzi wa data umefanywa kwa njia ya kimaelezo huku vitengo vikuu vya makosa ya kitahajia vikiwekwa wazi. Matokeo ya utafiti huu yatakuwa muhimu kwa walimu wa Kiswahili kwa kuwa yatatoa mwongozo wa kuwasaidia katika kutambulisha na kuainisha makosa ya kitahajia ya wanafunzi kama njia muhimu ya kuzua mikakati ya kupunguza utokeaji wa makosa katika mawasiliano andishi ya wanafunzi wao. Aidha, wanafunzi watapata maelekezo kuhusu mbinu za kutumia ili kuboresha uandishi wao kwa kuepuka makosa anuwai yanayochanganuliwa katika makala haya. Kwa usomi wa Kiswahili, makala itachangia kuweka misingi ya uchanganuzi wa makosa anuwai yanayojitokeza katika matumizi ya Kiswahili.