Lugha na Muktadha wa Matumizi yake katika Sekta ya Kilimo nchini Tanzania
Keywords:
Wingilugha, Lugha za Jamii, Uchanganyaji Lugha, Sera ya LughaAbstract
Mlolongo wa nyaraka za serikali, matamko na kauli za wanasiasa zinataja baadhi tu ya maeneo mahususi ya matumizi ya lugha Nchini Tanzania. Miongozo hiyo inaonekana kusisitiza zaidi hasa matumizi ya lugha katika mfumo wa elimu na mafunzo. Maeneo mengine ya utoaji wa huduma za jamii ikiwamo kilimo hayajapata kutolewa maelekezo kuhusu matumizi ya lugha. Matokeo yake ni vigumu kufahamu lugha gani inatumika katika muktadha upi wa utoaji wa huduma za kilimo. Hivyo, utafiti huu umechunguza lugha zinazotumika na muktadha wa matumizi yake katika sekta ya kilimo mkoani Morogoro nchini Tanzania. Kwa kutumia mbinu za hojaji, usaili na uchambuzi wa nyaraka, data zilikusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na katika matini za utoaji wa huduma za kilimo. Uchambuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya Ufanyaji Uamuzi ya Eastman (1983). Matokeo ya utafiti huu yanadhihirisha kwamba sekta ya kilimo inatawaliwa na hali ya wingilugha. Lugha zilizobainika kutumiwa katika utoaji wa huduma za kilimo ni Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kihispaniola, Kiluguru, Kipogoro, Kikagulu, Kinguu, na Kisagara. Hata hivyo, uwiano wa matumizi ya lugha hizo unatofautiana. Zipo lugha zinazotumika kwa kiwango cha juu na zingine kwa kiwango cha chini. Katika muktadha wa mashamba darasa lugha ya Kiswahili inatawala ilhali katika muktadha wa maduka ya pembejeo za kilimo na mfumo wa elimu na mafunzo, Kiingereza ndicho kinachotawala. Kwa hiyo, utafiti huu umehitimisha kuwa kuna haja ya kuwa na sera itakayoongoza matumizi ya lugha katika utoaji wa huduma za kilimo nchini Tanzania.