Matumizi ya Kiswahili katika Kuhamasisha Umma kuhusu Afya
Mtazamo wa Mawasiliano
Keywords:
Afya, mawasiliano, Kiswahili, kuhamasishaAbstract
Haja ya kuendeleza afya ya umma kwa kupambana na Virusi vya Ukimwi, Malaria na magonjwa mengine ni moja kati ya Malengo ya Milenia kuhusu Ustawi ambayo kila nchi inayoendelea inatazamia kutimiza kufikia mwaka 2015. Katika mpango wa muda mrefu wa maendeleo ya Taifa la Kenya (Kenya Vision 2030), Kenya inalenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kutoa huduma za kuzuia magonjwa katika kiwango cha vijiji na nyumba binafsi. Ili kufikia lengo hilo, ni muhimu kuwapa wananchi vijijini habari kuhusu magonjwa mbalimbali kwa kutumia lugha inayoeleweka na watu wengi, ambayo ni Kiswahili. Kwa hivyo, lengo kuu la makala haya ni kufafanua mbinu au michakato inayotumiwa kuwahamasisha wananchi kuhusu magonjwa mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili kwa mujibu wa nadharia ya mawasiliano. Wananchi huhamasishwa kwa kupashwa habari muhimu kama vile: majina ya magonjwa hayo kwa Kiswahili, vyanzo vya magonjwa, dalili zake na hatua za kujikinga. Habari hizo zinaweza kuchangia kuhamasisha umma kuhusu masuala ya afya na kuwawezesha kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali na hivyo basi kupunguza gharama ya matibabu nchini Kenya.