Dhima ya Viambishi Ngeli za Nomino za Ki-Vunjo
Keywords:
Dhima, Viambishi, Nomino, SemantikiAbstract
Makala haya yanashughulikia dhima ya viambishi ngeli za nomino za ki-Vunjo. Utafiti kuhusu makala haya ulifanyika Kaskazini Mashariki mwa Tanzania mkoani Kilimanjaro katika wilaya ya Moshi Vijijini. Mbinu ya Usampulishaji Nasibu Pangilifu ilitumika katika utafiti huu katika kupanga umri na jinsi, ambapo jinsi ya kike wamehusika watoa taarifa 15 na jinsi ya kiume wamehusika watoa taarifa 15. Watoa taarifa wote 30 walikuwa wazungumzaji wa ki-Vunjo wenye umri kati ya miaka 44-74. Taarifa zimekusanywa kwa watoa taarifa kwa kutumia njia za hojaji, usaili na ushuhudiaji. Utafiti huu ulilenga kubainisha dhima ya viambishi ngeli za ki-Vunjo. Ili kutimiza lengo hili, Mkabala wa Kisemantiki ulitumika sambamba na Nadharia ya Mofolojia Asilia (NMA) iliyopendekezwa na Dressler (1985) na Wurzel (1987). Matokeo ya utafiti huu yamebaini kuwa lugha ya ki-Vunjo ina idadi ya ngeli 18 ambapo imebainika kuwa katika viambishi ngeli kuna dhima mbalimbali zinazojitokeza zaidi ya umoja na wingi. Dhima hizo ni: ukubwa, udogo, uzuri na ubaya. Mwisho, utafiti huu umetoa mapendekezo ya tafiti fuatishi.