Utata baina ya Dhana za Unyambulishaji na Uambatizi katika Ufafanuzi wa Sarufi ya Kiswahili
Keywords:
Unyambulishaji, Uambatizi, Uambishaji, Mzizi, ViambishiAbstract
Makala hii imelenga kuibua utata uliopo baina ya dhana za unyambulishaji na uambatizi katika mofolojia ya Kiswahili. Unyambulishaji na Uambatizi ni dhana zinazohusu michakato ya uundaji wa maneno. Mgawanyo wa dhana hizi ulifanywa kwa kutumia chujio la lugha za Ulaya ambazo mofolojia yake ni tofauti na mofolojia ya lugha za Kibantu (Kosch, 2011). Hivyo, dhana hizo zinapotumika katika ufafanuzi wa sarufi ya lugha za Kibantu, kikiwemo Kiswahili, hubua utata. Makala hii imebaini kwamba utata huo husababishwa na mambo matatu. Kwanza, ni suala la dhima za viambishi vya unyambulishaji na uambatizi kuingiliana. Pili, ni suala la nafasi ya viambishi vya unyambulishaji na uambatizi katika mzizi au shina la neno. Tatu, ni kuwepo kwa istilahi tofauti tofauti zinazotumiwa na wanaisimu wa Kiswahili kurejelea dhana hizo. Makala hii imefafanua mambo hayo kwa kina na kuonyesha namna yanavyosababisha utata baina ya dhana ya unyambulishaji na uambatizi.