Ujitokezaji wa Uradidi katika Lugha ya Kihaya
Uchunguzi wa Kategoria ya Vitenzi, Vielezi na Vivumishi
Keywords:
Uelekeani, Uradidi, Vitenzi, Vielezi, VivumishiAbstract
Makala haya yanachunguza uradidi unavyojitokeza katika lugha ya Kihaya kwa kuangazia kategoria ya vitenzi, vielezi na vivumishi. Mtafiti amekusanya data ya makala haya katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Muleba Kata ya Izigo. Ameteua kata hii kwani ndiko inakozungamzwa Lahaja ya Kihamba inayoshughulikiwa na mtafiti wa makala haya. Halikadhalika, Kihaya kinatumiwa katika mawasiliano ya kawaida na shughuli nyingine nyingi za kiuchumi, kijamii nakadhalika. Mtafiti amekusanya data kwa kutumia mbinu za hojaji na uchambuzi wa matini. Mbinu ya kuchambua matini iliyotumika ni ile ya usomaji wa nyaraka za kitaaluma zilizompa mtafiti wigo wa kupata data faafu. Nyaraka zilizosomwa ni kama vile: tasnifu na maandiko mbalimbali. Hojaji hurejelea orodha ya maswali na maelekezo aliyoandaa mtafiti ambayo hujibiwa na watafitiwa, kwa lengo la kukusanya data faafu ya utafiti. Data ilichanganuliwa kwa kutumia mikabala ya maelezo na ufafanuzi. Aidha, makala haya yameongozwa na Nadharia ya Uelekeani iliyoasisiwa na McCarthy na Prince (1993, 1994a, 1994b na 1995). Matokeo ya makala haya yanaonesha kuwa uradidi hujitokeza katika kategoria za vitenzi, vielezi na vivumishi katika lugha ya Kihaya. Uradidi huo huweza kuhusisha neno zima au sehemu tu ya neno. Kwa vile makala haya yamechunguza sehemu tu ya uradidi katika lugha ya Kihaya, inapendekezwa utafiti ufanyike kuhusiana na kategoria nyinginezo kama vile nomino, vihusishi, vihisishi, viwakilishi nakadhalika.