Mchomozo wa Usitiari katika Lakabu za Watu Mashuhuri na Maarufu nchini Tanzania
Keywords:
Mchomozo, Lakabu, Usitiari, Majina, IsharaAbstract
Makala haya yanachunguza mchomozo wa usitiari katika lakabu za watu mashuhuri na maarufu nchini Tanzania. Lakabu ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipa kutokyana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo (Mulokozi, 2019). Majina haya ni maneno au mafungu ya maneno yenye maana iliyofumbatwa. Mara nyingi maneno au mafungu ya maneno hayo huwa na mchomozo wa usitiari ndani yake. Data ya makala haya kwa kiasi kikubwa imekusanywa maktabani kwa mbinu ya usomaji makini na kwa kiasi fulani uwandani kwa kuwasaili wanajamii kuhusu mchomozo wa usitiari katika lakabu hizo. Uchambuzi na uchanganuzi wa data umeongozwa na nadharia ya Jumuishi ya (Giles, 1979) na Nadharia ya Semiotiki (Saussure, 1976). Matokeo ya yanaonesha kuwa lakabu za watu mashuhuri na maarufu ni za kisitiari na zinabeba maana na ujumbe kuhusu ukweli ndani ya jamii husika. Hivyo, mchomozo wa usitiari unaojitokeza katika lakabu hizo unaibua dhamira za kisiasa, kijamii, kimajigambo na kiutamaduni. Kwa ujumla, uchunguzi wa makala unadhihirisha kuwa maumbile ya kimwili, nasaba na tabia au matendo ya mhusika vina nafasi kubwa katika utoaji wa lakabu za watu mashuhuri na maarufu katika jamii ya Watanzania.