Mitazamo ya Waafrika kuhusu Urithishwaji wa Mali
Uchunguzi wa Bunilizi za Kiswahili
Keywords:
Bunilizi, Urithi, Mali, Urithishwaji MaliAbstract
Kurithisha mali katika jamii nyingi za Kiafrika ni suala linalohifadhi na kuendeleza utamaduni wa jamii. Hivyo, thamani ya mwanadamu katika ulimwengu wake hubainika pia kupitia mali anazorithisha wengine. Vilevile, kupitia mali hizo, mrithishaji anaendelea kuishi katika fikra za wanaorithishwa hata baada ya kifo chake. Kwa msingi huo, urithishwaji wa mali ni hazina inayoendeleza kizazi na kuleta kumbukumbu idumuyo katika ulimwengu halisi wa mwanadamu. Fasihi ni akiso la maisha ya mwanadamu katika mazingira yake halisi. Kwa mantiki hiyo, bunilizi za Kiswahili huhifadhi na kudokeza misingi mbalimbali inayozingatiwa katika kuendesha maisha ya jamii. Mathalani, ile inayohusu suala la urithishwaji wa mali kupitia wahusika wanaosukwa kwa ustadi unaokidhi haja ya kufikisha maudhui lengwa. Hata hivyo, haijaelezwa bayana mitazamo ya Waafrika kuhusu suala la urithishwaji wa mali kwa kuhusianisha na bunilizi za Kiswahili. Hivyo basi, makala hii imeshughulikia jambo hilo kwa kujiegemeza katika riwaya za Rosa Mistika (1971) na Dunia Uwanja wa Fujo (1975). Makala hii ni matokeo ya data zilizopatikana maktabani kwa kutumia mbinu ya usomaji. Vilevile, katika uchunguzi, uchanganuzi na uwasilishaji wa matokeo hayo, misingi ya Nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi imetumika. Matokeo yanaonesha kuwa katika suala la urithishwaji wa mali kwa Waafrika, kuna mitazamo mbalimbali inayozingatiwa. Makala hii inajadili mitazamo mikuu mitatu, ambayo ni: mtazamo wa kitamaduni, kihiari, na kimabavu.