Ushairi na Umoja wa Kitaifa
Keywords:
Ushairi, Utenzi, Shairi, Uzalendo, Utaifa, UmojaAbstract
Ushairi ni utanzu mkongwe wa fasihi. Ulianza na binadamu mwenyewe alipobuni lugha (Fischer, 1953). Inadaiwa kuwa binadamu alianzisha ushairi alipovumbua lugha. Baada ya maendeleo ya mwanadamu, utanzu huu ulijijengea lugha ya kipekee ambayo ni ya mvuto na kunata. Kupitia lugha hii faida nyingi zinaweza kupatikana kwa matumizi yake. Faida mojawapo ni kuhamasisha jamii ya Wakenya kukubaliana, kuvumiliana na kupendana. Mtazamo huu unaleta umoja wa kitaifa ambao unahitajika sana nchini Kenya. Kenya imekuwa na tabia ya mgawanyiko mkubwa kila wakati wa uchaguzi mkuu na baada ya uchaguzi huo. Jambo hili lilitokea 2007/8, 2013 na 2017. Kuna njia nyingi za kukabiliana na tatizo hili. Mojawapo ni matumizi ya ushairi ulio na lugha ya nguvu sana inayowagusa watu katika sherehe na hafla mbalimbali. Unaweza kutumika kama nyimbo, maghani au katika maandishi. Utafiti huu kwa hivyo, unalenga kuchunguza ushairi unavyoweza kuchangia kuunganisha Wakenya wa jamii mbalimbali wanaoongea lugha tofauti tofauti. Kenya ina jamii arobaini na nne tukiongezea jamii ya Wamakonde iliyotambuliwa 2017 na serikali ya Jamuhuri ya Kenya. Utachunguza mashairi ya awali na tenzi zilizozungumzia umoja wa jamii na mashairi ya hivi punde kutathmini iwapo utanzu huu unaweza kuendeleza au kuchangia umoja wa kitaifa nchini Kenya.