Nafasi ya Kiswahili katika Mandhari-Lugha
Uchambuzi Kifani wa Mabango ya Matangazo ya Makampuni ya Mawasilino ya Simu
Keywords:
Mandhari-Lugha, Kiswahili, Makampuni ya Simu, Jiji la MbeyaAbstract
Tafiti zimeonesha kuwa kimatumzi, Kiswahili kinachukua nafasi ya pili katika maeneo ya umma ambayo katika makala haya hujulikana kama mandhari-lugha. Makala haya yametokana na utafiti wa uwandani uliofanyika katika Jiji la Mbeya nchini Tanzania mwaka 2018. Jumla ya mabango ya matangazo 156 ya makampuni ya mawasiliano ya simu yalikusanywa na kufanyiwa uchambuzi. Mabango ya matangazo ya makampuni ya mawasiliano ya simu yaliteuliwa kutokana na nafasi yake katika kutumia na kueneza lugha kwa haraka katika nyakati hizi za teknolojia ya mawasiliano. Uchambuzi ulifanyika kwa kutumia zanatepe ya Programu Tarakilishi ya Takwimu (PTT) katika kuainisha mipangilio ya lugha, mtawanyiko wa idadi ya maneno na ukubwa wa maandishi. Aidha, data za mahojiano na watumiaji wa simu na na baadhi ya mamlaka za serikali zimetumika kushadadia data za mabango ya matangazo. Kwa kutumia nadharia ya Ubeberu wa Kiisimu, matokeo yanaonesha kwamba Kiswahili kinajitokeza katika nafasi ya kwanza katika mandhari-lugha ya Jiji la Mbeya kwa vigezo vya mpangilio, idadi ya maneno na ukubwa wa maandishi. Matokeo haya yanatofautiana na tafiti zilizo nyingi ambazo hazikuzingatia idadi ya maneno wala ukubwa wa maandishi kama vipengele muhimu vya kueleza nafasi ya lugha katika mandhari-lugha. Vilevile, majina ya pekee katika uchambuzi yaliainishwa katika nafasi yake kwa sababu katika baadhi ya tafiti tangulizi majina ya pekee yamekuwa yakiathiri nafasi ya lugha na hali halisi ya wingilugha katika ikolojia. Pendekezo la makala haya ni kwamba tafiti zingine zifanyike katika mandhari-lugha ili kubainisha sababu za mandhari-lugha nchini Tanzania kutawaliwa na uwililugha suala ambalo linatishia wingilugha na uanwailugha.